BAADA
ya kuwatafuna `Kwalalumpa Malysia`, klabu ya Yanga ya Dar es salaam
mabao 3-2 jumapili ya wiki iliyopita, matajiri wa kuoka mikate, wana
Lambalamba, Azam FC wanaendelea kujifua vilivyo kuwakabili maaskari wa
jeshi la Magereza, Tanzania Prisons `Wajelajela` mwishoni mwa wiki hii
katika dimba la kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, mchezo wa ligi kuu
soka Tanzania bara.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka jijini Dar es salaam `Jiji la maji chumvi`,
Afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga amesema wanatambua ugumu
na ukongwe wa Prisons katika michuano ya ligi kuu, hivyo wanajipanga
kuhakikisha wanapambana kufa na kupona ili kupata pointi tatu muhimu
ugenini.
“Sisi
tunaendelea vizuri na mazoezi, lengo letu ni kupata pointi tatu muhimu.
Tunajua itakuwa mechi ngumu sana kwetu kwani Prisons wana uzoefu
mkubwa. Panapo majaaliwa tunaondoka kesho kuelekea Mbeya ili kuwaruhusu
wachezaji wetu kuzoea hali ya hewa ya jiji hilo ambayo ni ni tofauti na
Dar es salaam”. Alisema Jafar.
Mshambuliaji hatari wa Azam fc, John Raphael Bocco `Adebayor naye atakuwepo jijini Mbeya jumapili
Jafar
alifafanua kuwa wachezaji wote wako salama, wana morali kubwa kuelekea
mchezo huo ambao wanauheshimu sana kutokana na ugumu wa wajelajela
wanapokuwa katika dimba lao la nyumbani.
“Msimu
wa mwaka jana tulikutana na Prisons kwao na kuambulia pointi moja,
kiukweli ni wapiganaji sana wakiwa kwao, lakini sisi Azam fc kila mchezo
ni fainali kwetu, tuko tayari kupambana”. Alijigamba Jafar.
Kikosi cha Tanzania Prisons msimu uliopita ,(Picha na Makataba)
Wakati
huo huo, Maafande wa Tanzania Prisons wapo chimbo kujiandaa na kipute
hicho cha kukata na shoka kwa lengo la kupata ushindi wa kwanza baada ya
kufungwa mechi mbili ugenini, kutoka sare moja ugenini na mbili
nyumbani.
Katibu
mkuu wa Prisons, Inspecta Sadick Jumbe ametamba kuwaadibisha wana
lambalamba kutokana na kikosi chao chini ya kocha mkuu Jumanne Chale
kuimarika na kufuta makosa ya mechi za awali.
“Utakuwa
mchezo mgumu kwetu, Azam watachagizwa na ushindi walioupata dhidi ya
Yanga, tuko nyumbani na tutatumia vizuri nafasi hii kupata matokeo ya
ushindi na kuwafurahisha mashabiki wetu”. Alisema Jumbe.
Aidha
katibu huyo amewaomba mashabiki wa kandanda jijini hapa kujitokeza kwa
wingi katika mchezo huo ili kuwapa hamasa kubwa wanandinga wao.
Mbali
na mchezo huo wa jumapili (Septemba 29), kutakuwa na michezo mingine ya
ligi kuu ambapo Jkt Ruvu watakuwa dimba la Taifa jijini Dar es salaam
kuvaana na wekundu wa Msimbazi Simba.
Vibonde
wa ligi hiyo, wauza mitumba wa Ilala, Ashanti United watakuwa Azam
Complex mbande Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam kukwaruzana
na wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiania mkoani Morogoro, klabu ya
Mtibwa Sugar.
0 comments:
Post a Comment