Tuesday, September 24, 2013


PIX 6Maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani yakifunguliwa rasmi jana, watu 14 wamefariki dunia katika ajali mbili za zilizotokea katika mikoa ya Mbeya na Dodoma na wengine 25 kujeruhiwa.
Katika tukio la kwanza, watu sita wamefariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea barabara kuu ya Dodoma-Morogoro, eneo la Chinangali II wilaya ya Chamwino mkoani humo.
 Tukio la pili watu wanane wamekufa na wengine wanane kujeruhiwa katika ajali ya basi dogo iliyotokea jijini Mbeya juzi usiku.
Ajali hizo zinatokea wakati Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, akifungua maadhimisho ya wiki ya Usalama Barabarani jijini Mwanza ambako ameonya juu ya uzembe wa madereva barabarani.
Nchimbi alisema serikali haitavumilia uzembe wa madereva ambao umekuwa unasababisha ongezeko la ajali barabarani ambazo zimesababisha vifo na majeruhi. (Habari zaidi Uk. 3)
Akielezea ajali ya Dodoma, Kaimu Kamanda Polisi Mkoa huo, Damas Nyanda, alisema ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 3:30 usiku baada ya lori na basi kugongana uso kwa uso.
Alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha basi lenye namba T.433 BLR aina ya Youtong mali ya kampuni ya Al Sayed Express lililogongana na lori lenye namba T 102 CGR aina ya Leyland Daff lilokuwa na tela namba T 928 CHR.
Kaimu huyo alibainisha kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nizar Akran (45) na lori lilikuwa likiendeshwa na Hassan Mohamed (35) wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam, wote walifariki papo hapo.
PIX 7
“Basi lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuja Dodoma na lori lilikuwa likitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam na lilikuwa limebeba shehena ya mahindi na kusababisha vifo papo hapo kwa madereva wote pamoja na watu watatu waliokuwa katika lori hilo,” alisema Nyanda. Alitaja wengine waliofariki kuwa ni Ahmad Said (40) mmiliki wa lori, Hussen Rajabu (40), Imran Sharif (25) utingo wa lori wote ni wakazi wa Dar es Salaam. Hata hivyo, alisema abiria mmoja wa basi, mwanaume ambaye bado hajafahamika kwa jina mwenye umri kati ya 30-35 alifia hospitalini wakati akipatiwa matibabu.
“Baada ya kufariki vifo vimeongezeka na kufikia watu sita na majeruhi 17 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma,” alisema.
Alisema chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa basi uliosababisha kushindwa kulimudu, hivyo kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
Nyanda aliwataja majeruhi kuwa ni Anderson Mganga (33) kondakta wa basi, Raphael Ndonde (24), mkazi wa Dar es Salaam; Asanterabi Amani (25), Juma Yusuph(31), Abdul Msigwa (46) wote wakazi wa Dodoma; Magabuje Joseph (36), mkazi wa Moshi na Msafiri Mkauli (37), Godfrey Mhagama (28), wakazi wa Dar es Salaam.
Wengine ni Nyemo Matajiri (26), Silvia Matonya (60), Joyce Msuya (26), Fahazu Mohamed (25), Suzan Matonya (52), Sarafina Matajiri (24), Margareth Mongi (22), Lucy Nyomolele (21) na Rose Frederick.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Rufaa kwa utambuzi na uchunguzi wa madaktari. 
PIX 2. 
WANANE WAFA MBEYA
Katika tukio la pili, watu wanane wamefariki dunia kati yao watano wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa, baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace maarufu kwa jina la daladala, linalofanya safari zake kati ya Uyole na Majengo jijini Mbeya kufeli breki na kutumbukia mtoni.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:30 usiku katika eneo la Soko Matola jijini Mbeya, wakati basi hilo likielekea katika Kituo Kikuu cha Mabasi jijini Mbeya.
Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo walisema kuwa kabla ya kutokea kwa ajili hiyo waliliona gari hilo likiwa limepoteza mwelekeo na kuacha njia huku likiwa na mwendo mkali kuelekea mtoni. Mmoja wa mashuhuda hao, Jonas Schone, alisema kuwa aliliona gari hilo likipaa juu na kutua mtoni kabla ya kusikika kishindo kikubwa kutoka eneo la ajali.
Alisema baada ya kuona hivyo yeye na majirani walikimbilia katika eneo hilo na kukuta abiria waliokuwa ndani ya basi hilo wakihangaika kutoka, huku baadhi yao wakiwa wamepoteza maisha.
“Tulianza kuokoa watu waliokuwa ndani ya gari na tulitoa miili ya watu watano, kati yao wanawake walikuwa ni wawili na wanaume watatu, lakini miongoni mwa wanaume mmoja alikuwa ni mtoto mdogo,” alisema Sichone.
Kwa upande wake, Kisa Mwakalinga alisema aliliona gari hilo likipita kwa kasi jirani na nyumbani kwake na baada ya muda akasikia watu wakipiga kelele za ajali na ndipo alipokimbilia kwenye eneo la ajali na kukuta watu waliokuwa ndani ya gari hilo wakiwa wanatolewa na wasamaria wema mtoni, huku baadhi yao wakiwa wamekufa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, huku akilitaja gari lilipata ajali hiyo kuwa ni Toyota Hiace lenye namba za usajili T 223 AGQ.
Kamanda Diwani alisema kuwa watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni wanane kati yao wanaume wakiwa sita na wanawake wawili.
Kamanda Diwani aliwataja watu waliojeruhiwa ni Juma Warioba (32), mkazi wa Sae; Mwandela Mwamsi (22), mkazi wa Majengo; Kambi Ally (32), mkazi wa Iringa; Selemani Shelukindo, (25), mkazi wa Ileje; Nuru Shelukindo, (32), mkazi wa Ileje;  Bahati Ally (14), mkazi wa Songea na dereva wa basi hilo Dunia Francis. Kamanda Diwani alisema kuwa dereva wa gari hilo amekamatwa na hivi sasa anashikiliwa na Polisi wakati uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo ukiendelea.
DEREVA ASIMULIA
Akizungumza na NIPASHE akiwa wodini, chini ya ulinzi wa askari Polisi, dereva wa gari hilo, Francis alisema  wakati akiendesha gari hilo alisimama kwenye kituo cha daladala cha Soko Matola na alishusha abiria na kuendelea na safari ya kuelekea Stendi Kuu.
Alisema kuwa alipofika usawa wa kituo kidogo cha Polisi cha Mkapa, alikayaga breki na ndipo alipogundua kuwa gari lake limekatika breki na linazidi kuongeza mwendo.
Alisema kutokana na mwendo kuongezeka alishindwa kukata kona na badala yake akashika barabara ya vumbi kuelekea sehemu alikopata ajali.
“Mbele yangu niliona migomba nikaona kuwa nielekee huko ambako nilidhani naweza kusimama na kuokoa maisha ya watu, kwa vile sikuwa mwenyeji wa eneo hilo kumbe mbele kulikuwa na mto ndipo nikajikuta gari likitumbukia mtoni,” alisema Francis.
Katika ajali hiyo, baadhi ya watu walinusurika akiwamo mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye waokoaji wanadai kuwa walipofika eneo la ajali walimkuta mtoto huyo akiinuka na kutaka atoke nje ya gari hilo.
Miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa Mbeya na wito umetolewa kwa wananchi kwenda kuwatambua.
5 
WAKUU WA MIKOA WANENA
 Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa  Dar es Salaam ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amewataka wananchi , kuwakemea madereva wote wanaovunja kanuni na sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Sadiki aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema kuwa, ili kuimarisha usalama kwa Mkoa wa Dar es Salaaam, ni jukumu la kila mwananchi anayetumia barabara ili kupambana na vitendo vya uvunjaji wa sheria za barabara.
Pia Sadiki ameitaka Kamati ya Usalama Barabarani, kufanya kazi kwa kipindi cha mwaka mzima badala ya siku ya Maadhimisho pekee na kuendelea kutoa elimu katika vitongoji vyote hususan katika shule kwani watumiaji wakubwa wa barabara ni wanafunzi.
“Asilimia 25 ya vifo vya ajali za barabarani vinatokea zaidi kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15, na takwimu duniani zinaonyesha watu 500,000 wanakufa kutokana na ajali nyingi za ajali hizo zinatokea katika nchi zinazoendelea, ikiwano Tanzania,” alisema Sadiki.
1 
Ajali za barabarani zimeongezeka kwa mwaka huu. Kwa kipindi cha miezi sita iliyopita zimetokea ajali za barabarani 6,085 ambazo zimesababisha vifo vya watu 235, na majeruhi 3,997 ukilinganisha na mwaka jana zikiwa 5,424, na vifo 276, na majeruhi 2,366.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, ameiagiza Kamati ya Usalama Barabarani kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa kuandaa mafunzo kuhusu masuala ya usalama barabarani kwa walimu wa shule zote za msingi na sekondari ili kupunguza ajali.
Massawe alitoa kauli hiyo jana wakati akizundua wiki ya nenda kwa usalama barabarani ngazi ya mkoa wa Kagera.
“Kila shule ilete mwalimu mmoja ambaye baada ya kufundishwa atakwenda kuwafundisha wenzake na wanafunzi, ndipo tutapunguza matukio ya ajali anayozuilika,” alisema Kanali Massawe.
Alisema watoto wakifundishwa namna bora ya kutumia barabara ajali zitapungua kwa sasa na hata katika maisha ya baadaye maana nao watakwenda kuwafundisha wazazi na jamaa zao wengine wanaowaacha nyumbani.
Imeandikwa na Augusta Njoji, Dodoma; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Christina Mwakangale, Dar na Lilian Lugakingira, Bukoba.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video