Wakata Miwa wa mashamba ya Manungu Turiani Mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar kesho wanatarajia kuingia chimboni kwao Manungu Complex kujiandaa na mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu soka Tanzania bara katika uwanja wao wa nyumbani wa Manungu dhidi ya wana Lambalamba, Azam fc Agosti 24 mwaka huu.
Meneja wa klabu hiyo, David Bugoya ameiambia MATUKIO DUNIANI Kuwa kikosi cha Wana TamTam kilikuwa kimeweka kambi katika hoteli ya Itumbi Mwembechai jijini Dar es salaam na kesho inasafiri kurudi nyumbani kwao Manungu ili kunoa makucha yao na kupiga dua ya kuwafunga Azam fc waliowatungua katika uwanja wao msimu uliopita.
“Kikosi kipo salama, wachezaji wote wazima na kesho tunarudi Manungu kuendelea na mazoezi. Tutaanza ligi kuu kwa kuwakaribisha wazee wa Sauzi, itakuwa mechi ngumu sana kwetu lakini tutapambana kuvuna pointi tatu”. Alisema Bugoya.
Bugoya alisema kocha mkuu Mecky Mexime anaendelea kusuka kikosi chake hasa safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Juma Luizio na Abdallah Juma, huku kiungo mshambuliaji fundi Shaban Kisiga “Marlone” akiwa nyuma yao na kufanya kazi nzuri.
“Ni wakati wa maandalizi, mashabiki wasahau yanayotokea katika mechi za maandalizi, kocha anajaribu wachezaji wake ili kupata kikosi cha kwanza cha kuanzia ligi kuu”. Alisema Bugoya.
Miaka ya nyuma ilikuwa ngumu sana kwa wapinzani kupata matokeo ya ushindi kutoka kwa Mtibwa Sugar katika dimba la Manungu Complex, lakini miaka ya hivi karibuni wana TamTam hao wamekuwa mboga kweli kwani huwa wanachezea vichapo vya kutosha.
0 comments:
Post a Comment