Na Boniface Wambura, TFF
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Yanga na Taifa Stars, Baraka Kitenge (74) kilichotokea leo mchana (Agosti 20 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kitenge akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
Kitenge amefia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa akisumbuliwa na kansa ya uti wa mgongo. Enzi zake katika Yanga na Taifa Stas alicheza na wachezaji kama akina Athuman Kilambo na Abdulrahman Juma.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kitenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa Marehemu, Yombo Vituka (Jet) jijini Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Kitenge mahali pema peponi. Amina
0 comments:
Post a Comment