Na Baraka Mpenja
Kufuatia kuondoka kwa kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula aliyetimkia Qatar ambapo amefanya majaribio katika klabu ya Al Markhiya Sports Club ya Doha na kufuzu, leo hii wekundu wa msimbazi, Simba wamemsainisha kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kusaka Kabumbu Mzanzibar, Abdulhalim Humud maarufu kwa jina la ‘Gaucho’ wa kibongo bongo.
Nyota huyo aliyekuwa anakipiga Azam fc aliuzwa katika klabu ya Jomo Cosmos ya Bondeni Afrika Kusini, lakini akaamua kukacha na kurejea nyumbani na kwenda kufanya majaribio Msimbazi ambapo alifuzu na leo hii mbele ya makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Joseph Itang`are “Kinesi” ameanguka saini mkataba wa miaka miwili.
Humud ataungana na viungo mahiri wa Simba akiwemo Kinda Abdallah Seseme, Amri Kiemba “Fundi” na wengineo kuimarisha safu ya kiungo ya klabu hiyo.
Mchezaji huyo mwenye mwili wa mpira, anasifika kwa uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga pasi za uhakika, lakini mpira wa kutumia nguvu ndio mahala pake.
Mbali na nyota huyo, pia Simba wamemsainisha beki wa kati kutoka klabu ya Abajalo ya Sinza jijini Dar es salaam, Rahim Juma kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kufuzu majaribio mbele ya kocha mahiri na winga machachari wa zamani wa Simba, Abdallah King Kibaden “ King Mputa”.
Wakati huo huo taarifa za ndani kutoka ndani ya uongozi wa Simba zimedokeza kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Simba kutoka nchini Burundi na mfungaji bora wa michuano ya kombe la Kagame mwaka huu , Amis Tambwe anaingia leo usiku jijini Dar es salaam tayari kwa kujiunga na kambi ya Simba iliyopo maeneo ya Bamba Beach Kigamboni jijini Dar es salaam.
Akiongea na mtandao huu kwa masharti ya kutotajwa jina, kiongozi huyo alisema Tambwe ataingia leo, wakati Moses Oloyo anatarajia kuingia mwishoni mwa mwezi kujiunga na Simba.
Tambwe tayari alishasaini mkataba wa miaka miwili siku za nyuma na alirejea kwao kwa mapumziko na maandalizi ya kuhamia jiji la maji chumvi, Dar es salaam kwa ajili ya kazi yake ya kuitumikia Simba.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa sasa majina ya wachezaji wote waliosajiliwa na Simba yanafanyiwa kazi na kupelekwa shirikisho la soka Tanzania kwani siku ya mwisho ya usajili ni Agosti 3.
0 comments:
Post a Comment