Wekundu wa Msimbazi , Simba wameendelea na harakati zao za kutafuta beki mzuri wa kati, na leo hii wamemsajili beki wa kimataifa raia wa Uganda, Joseph Owino Gella kwa mkataba wa miaka miwili.
Owino amesaini kwa mara nyingine Simba kwani aliwahi kuitumika klabu hiyo kabla ya kuachwa na kujiunga na klabu ya Azam fc ambapo alishindwa kulishawishi benchi la ufundi la wana lambalamba na akaamua kurejea kwao Uganda na kujiunga na miamba ya soka nchin humoi, wakusanyaji wa mapato wa URA.
Beki huyo mwenye uwezo mkubwa wa kusimama katika safu ya ulinzi, amesaini mkataba huo mbele ya makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Joseph Itang`are maarufu kwa jina la “Mzee Kinesi” na mjumbe wa kamati ya utendaji Said Pamba.
Owino aliyekuwa anaichezea klabu ya URA aliwavutia viongozi wa Simba wakati wa mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya URA katika uwanja wa Taifa ambapo Mnyama alilala 2-1, hivyo benchi la ufundi likaagiza nyota huyo asajiliwe na ndipo mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Kapteini Zacharia Hans Poppe akamfuata na kuongea naye.
Mbali na mchezo huo, Owino alionesha kiwango cha juu katika mchezo dhidi ya Yanga ambao walitoka sare ya 2-2 huku wanajangwani wakisawazisha dakika za lala salama. Pia katika mechi dhidi ya Coastal Union uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo URA walilala 1-0, nyota huyo mwenye umbo la mpira alionesha ufundi mkubwa na kuendelea kuwachanganya viongozi wa Simba.
Akiwa jijini Dar es salaam wakati klabu ya URA ilikuwa katika ziara ya kucheza mechi tatu nchini, Owino alikaririwa akisema yupo tayari kurejea Simba kwani ni kama nyumbani, hivyo aliwakaribisha katika mazungumzo na ndipo Hans Poppe akaonesha umahiri wake katika usajili leo hii amemwaga wino Msimbazi.
Kutokana na usajili huo, beki mwingine raia wa Uganda, Samuel SSenkoom ametolewa kafara na sasa Simba kidogo roho zao zinatulia baada ya kulamba dume la uhakika.
Tangu mabeki Kelvin Yondan kuihama Simba na kujiunga na Yanga, wakati Juma Nyosso hakuwa katika uhusiano mzuri na viongozi, safu ya ulinzi imekuwa uchochoro sana na msimu uliopita safu hiyo ilishindwa kuhimili mikikimikiki ya ligi kuu na ligi ya mabingwa barani Afrika ambapo walitolewa hatua ya mwanzo.
0 comments:
Post a Comment