Na Eleuteri Mangi – MAELEZO), Dar es Salaam
Serikali imeanzisha mkakati wa kutokomeza wimbi la tatizo la dawa za kulevya nchini kwa kudhibiti viwanja vya ndege na sehemu mbalimbali za mipakani zinazotuhumiwa kupitisha dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Assah Mwambene leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara hiyo.
“Kwa yeyote aliyekuwa anafikiria kufanya biashara ya dawa za kulevya ajue muda wake umekwisha” alisema Mwambene.
Mwambene alisema kuwa tatizo hili litakuwa historia kwani ulinzi umeimarishwa, hivyo ametoa rai kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufanya biashara hiyo aache mara moja.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa Serikali imeweka jitihada kubwa ya kutoa elimu kwa watumiaji na waathirika wa dawa za kuelevya ili waweze kubadili tabia zao za kutumia dawa hizo na kuwa watu wema katika jamii.
Aidha Mkurugenzi Mwambene amekanusha taarifa zilizoandikwa kwenye mtandao wa “twitter” kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni shemeji wa aliyekuwa Rais wa Rwanda Juvenal Havyarimana.
“Taarifa hizi haina ukweli wowote na zinalenga kumpaka matope Rais Jakaya Mrisho Kikwete”, ameongeza Mwambene.
Assah Mwambene amefafanua kuwa lengo la mitandao ya kijamii ni kuhabarisha na kuelimisha Umma na si kupotosha jamii kwa kuandika habari zisizo na ukweli wowote.
0 comments:
Post a Comment