Msimu uliopita kikosi hiki (pichani) kilihangaika kukwepa rungu la kushuka daraja chini ya kocha msaidizi Greyson Haule, lakini msimu ujao kitaongozwa na kocha mpya Mbwana Makata akisaidiana na Haule na tayari ameshaanza kazi ya kukisuka kikosi chake
………
Na Baraka Mpenja
Kocha mpya wa maafande wa JKT Ruvu wenye makazi yao Mkoani Pwani, Mbwana Makata amesema kikosi chake hakichabadilika sana kwani wachezaji wengi ni walewale waliokuwepo msimu uliopia, lakini anafanya kazi ya kubadili mfumo wa uchezaji katika kikosi chake.
Akizungumzo na mtandao wa MATUKIO DUNIANI leo hii, Makata amesema kuifundisha klabu hiyo ni changamoto nyingine kwake kwani mashabiki wa soka mkoani Pwani wanatarajia mafanikio makubwa kutoka kwake, ila hana wasiwasi kwani anajua mfumo wa timu za majeshi.
“Nazijua timu za Majeshi, msimu uliopita nilikuwa na JKT Oljoro, sasa nipo na JKR Ruvu, naweza kusema kikosi changu ni kizuri, hivyo msimu ujao nitahakikisha napambana kupata mafananikio mapema kuliko kusubiri dakika za lala salama na kutafuta njia ya kubakia”. Alisema Makata.
Kocha huyo alisema asubuhi ya leo alikuwa na kikosi cha wakubwa katika mazoezi, lakini mchana huu wakubwa wamepumzika na anaedelea na mazoezi ya kikosi cha chini ya umri wa miaka 20.
“Unajua usajili wa timu ya wakubwa unaenda sambamba na wa timu ya chini ya umri wa miaka 20, hivyo kwa sasa nipo nao hapa uwanjani nikiangalia namna ya kukisuka kikosi hiki kwa kufanya usajili mzuri, kwani nikiwa na kikosi kizuri cha vijana itakuwa rahisi kwangu kuwapandisha kwenda timu A”. Alisema Makata.
Kocha huyo aliongeza kuwa msimu ujao anatarajia kuwashangaza wengi kutokana na uzoefu wake, lakini bado amelia na waamuzi wa ligi kuu ambao msimu uliopita walilalamikiwa sana kutokana na vitendo vyao vya kuchezesha chini ya kiwango.
“Tatizo la waamuzi limekuwa changamoto kubwa sana katika ligi yetu, lakini nadhani waamuzi wetu wanajua sana kutafsiri sheria 17 za soka, kinachowasumbua wakati mwingine ni unazi wa timu fulani, ila kama watazingatia weledi wa kazi yao, nina hakika tutafanya vizuri sana”. Alisema Makata.
Makata ataiongoza klabu ya JKT Ruvu Kufungua pazia la ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mgambo JKT, uwanja wa chama cha mapinduzi, Mkwakwani, jijini Tanga.
0 comments:
Post a Comment