Na Baraka Mpenja
Kocha mkuu wa wapiga kwata wa Mkoani Pwani, klabu ya Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa “Masta” amesema kufungwa katika mechi za kirafiki wakati huu wa maandalizi ya ligi kuu soka Tanzania bara ni suala la kawaida kwani anawapima wachezaji wake, hivyo mashabiki wasichanganyikiwe hata kidogo.
Mkwasa alisema kwa sasa anawapima wachezaji wapya aliowasajili, ingawa baadhi ya wachezaji wanashindwa kujituma hususani baada ya kukamilisha usajili wao, lakini anajitahidi kuwadhibiti ili kufanya kile alichokusudia msimu ujao.
“Unajua wakati huu wa maandalizi hutakiwi kukosana na mchezaji, kila mchezaji lazima apate haki ya kujaribiwa, nafanya kila liwezekanalo kuwapima wachezaji wangu, lakini kasumba ni ile ile kwa wachezaji wa Kitanzania, wanazembea sana katika mazoezi na hii ndio sababu kubwa ya kushindwa kung`ara kwa muda mrefu”. Alisema Mkwasa.
Mkwasa aliongeza kuwa licha ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki na kufungwa, lakini kikosi chake kinaimarika zaidi na kuonesha matumaini ya kushika nafasi tatu za juu msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi Agosti 24 mwaka huu.
“Lengo letu na kutwaa ubingwa kwa sababu uwezo huo tunao, mtu anayefuatilia soka la Tanzania anajua jinsi tunavyoonesha kiwango cha juu, msimu ujao tunajipanga kufika mbali zaidi ikizingatiwa tumesajili wachezaji wazuri akiwemo Elias Maguli na Stephano Mwasyika”. Aliongeza Mkwasa.
Hata hivy, Mkwasa hakusita kuwanyooshea kidole waamuzi wa ligi kuu kwa madai ya kuwa wanachezesha chini ya kiwango na kuzigharimu baadhi ya timu wakiwemo wao, hivyo lazima wajitahidi kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka na wasitumiwe na baadhi ya timu kupanga matokeo.
Ruvu Shooting wataanza mbio za kuwania ubingwa au nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi kuu kwa kuoneshana kazi na maafande wa Tanzania Prisons “Wajelajela” kutoka jijini Mbeya katika uwanja wao wa nyumbani wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani Agosti 24 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment