Na Baraka Mpenja kwa msaada wa Sportsmail.com
KOCHA wa Manchester United, David Moyes amejiingiza katika mbio za kumuwania kiungo mshambuliaji raia wa Brazil, Willian, kwa dau la uhamisho la pauni milioni 30 ili ajiunge na ligi kuu soka nchini England.
Mchezaji huyo anayekipiga katika klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi tayari ameshazivutia klabu za Liverpool na Tottenham, lakini Manchester United wanaonekana kuwa na uwezo zaidi wa kuzipiku.
Liverpool tayari wamefikia hatua kubwa ya mazungumzo na Anzhi ili kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 na kilichobaki ni makubaliano ya ndani. Lakini United wameshaingia katika kinyang`anyiro hicho na Old Trafford inaaminika kuwa kivutio kikubwa kwa Willian.


Tottenham wamekuwa wakimuwania sana mchezaji huyo wa zamani wa Shakhtar Donetsk na wapo tayari kumchukua kwa gharama kubwa ikizingatiwa kuwa mshambuliaji wao tegemeo Gareth Bale yuko katika hatua za mwisho kukamilisha dili la kujiunga Bernabeu.
Willian ameiambia ESPN anaweza kufungua mazungumzo na Liverpool, akisema: ‘Kulikuwa na dili la Manchester City, lakini likabumburuka. Sasa nasubiri ofa nyingine kutoka klabu mpya siku zijazo, klabu kama Liverpool. Kama kweli itakuwa Liverpool, daah! kiukweli ni klabu kubwa. Nina matumaini na nitatulia kusubiri mafanikio makubwa”.
“England ndio mipango yangu. Napenda sana ligi ya nchini humo, nafurahia soka la England, kama itatokea nikapata nafasi, itakuwa nafasi nzuri kwangu na taswira yangu ya kisoka kwa ujumla”.
United wanataka kusajili jina kubwa zaidi majira haya ya kiangazi, na wameshatuma ofa kwa Real Madrid wakihitaji kumsajili nyota wao, Raia wa Ujerumani, Mesut Ozil kwa dau la uhamisho la pauni milioni 40.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka , 24, alikuwa katika mawindo ya Sir Alex Ferguson baada ya fainali za kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini, lakini akajiunga na Real Madrid kwa dau la pauni milioni 12.5. Sasa yuko tayari kuihama miamba hiyo ya soka la Hispania.

0 comments:
Post a Comment