Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Mbeya
Ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 imezidi kuchanganya zaidi kwa timu zote 14 kushuka dimbani leo hii katika viwanja saba nchini.
Mechi iliyokuwa na msisimko zaidi ni ile ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Klabu ya Yanga ya Dar es salaam dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mechi hiyo imemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya 1-1.
Huko Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mnyama Simba amewagalagaza wenyeji wa uwanja huo,maafande wa kupiga kwata wa JKT Oljoro bao 1-0.
Wana lambalamba, Azam fc walikuwa wageni wa maafande wa Rhino Rangers na kushuhudia wakali hao wa Chamazi wakipata ushindi wa mabao 2-0.
JKR Ruvu ya Pwani imewabamiza mabao 3-0 Tanzania Prisons katika uwanja wao wa nyumbani wa mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
Nao Mgambo JKT wameibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wauza mitumba wa Ashanti United katika dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Wana TamTam wa mashamba ya miwa ya Manungu Turiani Mkoani Morogoro wamewakaribisha watengeneza sukari wa Kaitaba mkoani Kagera na kushinda bao 1-0 na kufuta makosa ya kutoka sare ya 1-1 na Azam fc mechi ya ufunguzi.
Hapa jijini Mbeya ambapo jicho la FULLSHANGWE kitengo cha habari za michezo na burudani kiliweka kambi yake, wenyeji wa Uwanja wa sokoine, klabu ya Mbeya imewafunga wageni wao Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani mabao 2-1.
Mabao ya Mbeya City yalifungwa dakika ya saba ya kipindi cha kwanza na Paul Nonga, wakati katika dakika ya 25 kipindi hicho, Shooting walisawazisha bao hilo kupitia kwa Shaban Susaz.
Bao la ushindi kwa Mbeya City lilitiwa kimiani na mshambuliaji wao hatari Steven Mazanda dakika ya 93 na kuleta shangwe kubwa kwa mashabiki waliofurika uwanjani.
Baada ya kumaliliza kwa mechi hiyo, kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema timu yake bado ni ngeni ligi kuu, hivyo mashabiki wawape nafasi wachezaji wao na kuacha tabia ya kuwazomea kama walivyofanya leo.
“Timu ndio inaanza ligi kuu, hii ni mechi ya pili, mashabiki wamenikera sana kwa kuwazomea wachezaji na kushinikiza mambo yasiyowezekana, hakika wanatakiwa kuacha tabia hii kwani si nzuri na timu inatakiwa kupewa muda zaidi ili kujipanga”. Alisema Mwambusi.
Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa “Masta” akiongea na waandishi wa habari baada ya kupoteza mchezo wa leo dhidi ya Mbeya (picha na Habari Online blog)
Kwa upande wa Kocha wa Shooting, Charles Biniface Mkwasa “Masta” amesema mchezo huo haukuwa mzuri kwake kwani wachezaji walishindwa kutulia na kuonesha soka alilotarajia.
“Kiukweli mpira ulikuwa mgumu sana, wachezaji wamecheza tofauti na nilivyodhani, hata hivyo waamuzi wamekosea sana dakika za mwisho, waliongeza dakika tano, mtu ameanguka, ikiwa imebakia dakika moja mpira kumalizika, ghafla mwamuzi ilipuliza kipenga cha mwisho.” Alisema Mkwasa.
Ligi kuu itasimama mpaka septemba 14 mwaka huu ambapo imepisha kambi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inayoanza kesho agosti 29, kujiandaa na mechi ya kukamilisha ratiba ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil ugenini dhidi ya Gambia.
0 comments:
Post a Comment