Na Baraka Mpenja
“Wanankulukumbi”, Kagera Sugar wenye makazi yao uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera wanatarajia kuondoka wiki ijayo kuelekea nchini Uganda ambapo watacheza mechi tatu za kujipima ubavu kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaoanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu.
Akizungumza na mtandao wa MATUKIO DUNIANI mchana huu, Afisa habari wa klabu hiyo, Hussein Mohamed amesema kocha mkuu wa kikosi hicho, Mganda, Jackson Mayanja tayari ameshaondoka kwenda nchini Uganda kurekebisha mipango ya ziara hiyo ambayo lengo lake ni kujaribu wachezaji wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu mpya.
“Awali nilizungumza na mtandao huu na kueleza kwamba tumepata mwaliko Kisumu Kenya kwenda kushiriki michuano ya Viwanda vya Sukari, lakini wenzetu wamesogeza mbele, hivyo tumeona itatubana sana kutokana na kujiandaa na ligi kuu, hivyo tumeamua kwenda Uganda kujipima uwezo”. Alisema Hussein
Hussein alisema wakiwa na Uganda watacheza mechi tatu za kirafiki ambapo mechi ya kwanza itakuwa dhidi ya KCC, ya pili itakuwa dhidi ya Sports Club Villa, majogoo wa Kampala na mechi ya mwisho watachuana na wakusanyaji wa mapato wa URA.
“Tukishacheza mechi hizo, tutarejea nchini kuendelea na mazoezi ya mwisho kabla ya kuanza ligi kuu. Kocha wetu ni mzoefu na ana kiwango kizuri cha kufundisha, hivyo tutafanya vizuri sana”. Alisema Hussein.
Afisa habari huyo alisema msimu ujao wanatarajia kufanya vizuri zaidi na kushika nafasi tatu za juu, licha ya kuongozwa na kocha mpya.
Kagera Sugar wataanza ligi kuu soka Tanzania bara Agosti 24 mwaka huu kwa kupambana na timu mpya ya Mbeya City chini ya kocha Mwambusi katika uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
0 comments:
Post a Comment