Maafande wa Jeshi la kujenga Taifa, JKT Ruvu wa mkoani Pwani wametamba kuendeleza dozi msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kuibuka kidedea katika mechi zao mbili za kwanza .
Maafande hao chini ya kocha mkuu, Mbwana Makata walianza ugenini agosti 24 dhidi ya Mgambo JKT na kushinda kwa 2-0 na hapo jana walishinda mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Mabatini Mlanndizi Mkoani Pwani.
Akizungumza kwa njia ya Simu na Mtandao wa FULLSHANGWE, kocha msaidizi wa kikosi hicho Greyson Haule amesema baada ya mechi ya hapo jana wamepanda kileleni mwa msimamo wa ligi kuu wakijikusanyia pointi 6 bila kufungwa bao lolote, lakini mipango yao ni kuendelea kutoa vipigo kadri Mungu atakavyowajalia.
“Tumejipanga kufanya vizuri sana msimu huu, vijana wana morali kubwa sana na wanafuata maelekezo ya makocha wao. Kama kikosi kitakuwa na kiwango kilichoonekana mechi mbili za nyuma, hakika tutafanya makubwa na kuwashangaza wengi tofauti na msimu uliopita ambapo tulikuwa tunapumulia mashine”. Alisema Haule.
Kocha huyo alisema kocha mkuu, Makata amekuwa chachu kubwa kwa wachezaji , kwani kiwango chake cha ufundishaji kipo juu sana na ndio maana vijana wanaelewa na kufanyia kazi mafundisho yake.
“Tangu aje Mwalimu Makata, Jkt Ruvu imebadilika na kucheza soka safi na la ushindani, wapinzani wetu wajiandae vizuri, wembe tuliotumia kuwanyoa Mgambo mechi ya ufunguzi na Tanzania Prisons hapo jana utaendelea kutumika mechi zinazofuata”. Alisema Haule.
Pia kocha huyo aliwataka mashabiki wa soka mkoani Pwani kuendelea kuwaunga mkono zaidi ili wafikie malengo yao, huku akitoa wito wa kuwa wavumilivu na kujitokeza kwa wingi mara timu hiyo inaposhuka dimbani.
Mkoa wa Pwani unawakilishwa na timu mbili katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara, JKT Ruvu na Ruvu Shooting ambayo hapo jana jijini hapa ilifungwa mabao 2-1 na wageni wa ligi kuu, klabu ya Mbeya City, ingawa katika mechi ya kwanza waliwapiga Prisons risasi 3-0.
0 comments:
Post a Comment