Matajiri wa soka la Tanzania kwa sasa, wana lambalamba Azam fc wanatarajia kukwea pipa kesho majira ya saa tano asubuhi uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam kuelekea nchini Afrika kusini ambako wataweka kambi ya siku kadhaa.
Meneja wa Azam fc, Jemedari Said amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na wakiwa huko watacheza mechi kadhaa za kujipima uwezo na watarejea nchini Agosti 13 mwaka huu ikiwa ni siku chache kabla ya kucheza mechi ya ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2013.
Said alisema wanatarajia kucheza mechi na miamba ya soka la Afrika Kusini kwa maana ya Supersport United, Orland Pirates, Amazulu na nyinginezo, lengo likiwa ni kupata uzoefu na changamoto mpya kabla ya kuanza kuusaka ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara na michuano ya kombe la shirikisho.
“Ziara ya Afrika kusini itakuwa na manufaa sana kwetu, wenzetu wameendelea sana kisoka, hivyo tutapata changamoto nzuri ya kujiandaa na michuano inayotukabili siku za usoni”. Alisema Said.
Azam fc wanakabiliwa na michunao ya kimataifa mwakani, hivyo lazima wakae kidete kuandaa kikosi chao kilichosheheni nyota wa hapa Tanzania na nje ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment