Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mechi ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa Julai 18 mwaka huu.
Klabu ya Yanga inataraji kucheza mechi ya kimataifa ya Kirafiki dhidi ya timu ya 3 Pillars ya Nigeria itakayochezwa Julai 18 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya klabu zote mbili kabla ya ligi kuu kuanza mwezi ujao ambapo Yanga pia inajinoa kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Mratibu wa mechi Salum Mkemi amesema kikosi cha wachezaji 17 na viongozi na makocha wao wapo jijini Dar es Salaam wakijifua kwa ajili mtanange huo utakaochezwa katika uwanja wa Taifa.
Mkemi amesema pia timu ya 3 Pillars ambayo imepanda daraja la ligi kuu nchini Nigeria inataraji kujipima na Coastal Union ya Tanga huku wakifanya mazungumzo na Mbeya City kwa ajili ya mechi nyingine za Kirafiki.
Katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako amesema wachezaji wako kambini kujiwinda na michuano ya ligi kuu na kuongeza kuwa wana morali kuelekea mchezo huo.
Mratibu wa mechi ametangaza Viingilio vya mechi hiyo vitakuwa kati ya shilingi elfu tatu na elfu 15 ili kuwawezesha mashabiki wengi zaidi kuhudhuria kipute hicho.
Timu ya 3 Pillars inataraji kurejea nchini Nigeria Julai 30 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment