Hili Taji litaenda wapi msimu ujao?, je, wanajangwani wataweza kulibakisha au litaenda kwa wanaume wengine?, Tusubiri safari inayoanza Agosti 24 mwaka huu
………………..
Na Baraka Mpenja
Mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga ya Dar es salaam inaendelea kujifua vilivyo katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es salaam kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ambapo wataanza kibarua chao Agosti 24 dhidi ya wageni, Ashanti United “wauza Mitumba” katika dimba la Taifa jijini Dar e salaam.
Afisa habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto ameiambia MATUKIO DUNIANI kuwa kwa sasa wanamshukuru Mungu kwani wachezaji wote ni wazima na wanaendelea vizuri na mazoezi, huku wakiahidi kutowaangusha mashabiki wao kwa kutetea ubingwa wao msimu ujao.
“Kikosi kinaendelea salama, program zote mwalimu ndiye mhusika, lakini ninachoweza kukwambia ni kuwa mazoezi yanaendelea na kocha anaahidi kutengeneza kikosi cha ushindani kwa ajili ya ligi kuu pamoja na michuano ya kimataifa”. Alisema Kizuguto.
Kizuguto alisisitiza kuwa Yanga wana majukumu ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, na lengo lao kubwa ni kufuta uteja wa timu za Tanzania katika mchuano ya kimataifa.
“Tumesajili vizuri sana, kikosi kipo kamili. Unajua Yanga ndio timu bora kwa sasa, wachezaji wanajitambua na kujituma zaidi mazoezini, kwahiyo mashabiki waelewe kuwa tunajiandaa kwa nguvu zote na lazima tufike mbali”. Alisema Kizuguto.
Wakati mazoezi yakiendelea vizuri, lakini bado kuna utata juu ya mchezaji nyota wa klabu hiyo, Hamis Kiiza ambaye mpaka sasa kuna taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo kuwa amerejea tena kwao Kampala baada ya kushindwa kuelewana juu ya dau la usajili.
Lakini mpaka sasa Yanga hawana wasiwasi baada ya kumnasa Hussein Javu kutoka Mtibwa Sugar ambapo usajili wa nyota huyo umekamilika na sasa anaendelea kujinoa na wanajangwani uwanja wa Loyola.
Mbali na Javu, katika safu ya ushambuliaji kuna bunduki nyingine, Jerryson Tegete, Didier Kavumbagu na shaban Kondo.
Yanga mpaka sasa wamecheza mechi za kirafiki nne tangu waanze maandalizi ya ligi kuu, na kati ya hizo wamefungwa moja na kutoka sare tatu.
0 comments:
Post a Comment