Na Baraka Mpenja
Wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani Mji kasoro bahari, Morogoro, klabu ya Mtibwa Sugar wamepata mwaliko nchini Kenya wa kushiriki mashindano ya Viwanda vya sukari yatakayofanyika Kisumu mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Mwenyekiti wa Mtibwa, Jamal Baiser amesema wanachokifanya kwa sasa ni kuwasiliana na Wakenya ili kujua watapata nini na watajitegemea kwa mambo gani na baada ya hapo wataamua kwenda.
“Ni kweli tumepata mwaliko, kwa sasa tunazungumza nao ili kujua wao watatupatia nini na tutajitegemea kwa mambo gani, lakini nia yetu ni kwenda huko kwani itakuwa nafasi nzuri ya kujiandaa na ligi kuu soka Tanzania bara. Siku zote tunachotaka ni mechi nyingi za majaribio, hivyo mambo yakiwa sawa lazima tukashiriki”. Alisema Baiser.
Baiser alisema kwa sasa wanaendelea na mazoezi vizuri na wachezaji wote wapo salama, huku akiweka wazi kuwa wamepata pengo baada ya kumpoteza mshambuliaji wao Hussein Javu aliyejiunga na Yanga.
“Javu hatunaye tena, lakini tuna kijana Kinda tuliyempandisha, mshambuliaji wa timu ya taifa Juma Luizio, lakini tumeongeza nguvu kwa kumsajili mshambuliaji aliyekuwa klabu ya Simba, Abdallah Juma, kwa hiyo wawili hawa wataimarisha safu yetu ya ushambuliaji”. Alisema Baiser.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa lengo lao kwa msimu ujao ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara na wataanza mitanange hiyo kwa kuvaana na makamu bingwa wa ligi hiyo, wana lambalamba , Azam fc Agosti 24.
Wakati Mtibwa wakijipanga kwenda Kisumu Kenya, wapinzani wao wa kwanza wa ligi kuu wanatarajiwa kuondoka nchini Agosti 2 kwenda Afrika kusini kuweka kambi ya wiki mbili na watajipima ubavu na miamba ya soka la huko, Orland Pirates, Supersport United na nyinginezo.
0 comments:
Post a Comment