HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Raia wawili kutoka nchi jirani ya Kenya Bw. Robert Mwadime Mwakana (30) na Bw. Dickson Kawa Mbole (27) wamekamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro tarehe 13.07.2013 bila kuwa na kibali cha kupanda Mlima Kilimanjaro.
Raia hao wanaotoka eneo la Taveta nchini Kenya wanasadikiwa kuingia Hifadhini kwa
kupitia vichakani na walikamatwa kati ya eneo la Lango la Marangu na Kituo cha Mandara. Suala hili tayari limeshafikishwa kwa Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro kwa hatua
zaidi za kisheria.
Aidha, katika hatua nyingine watu watatu wa familia moja wamekamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakishirikiana na polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali ambazo ni mifupa mitatu ya twiga yenye uzito wa kilo 10.4 na mfupa mmoja wa tembo wenye uzito wa kilo tano.
Watuhumiwa hao Charles Mollel, Alex Tukai Mollel na Samwel Tukai Mollel walikamatwa katika eneo la Kisongo Olasite kufuatia taarifa kutoka kwa raia wema juu ya watuhumiwa kumiliki nyara hizo. Vile vile askari wa Hifadhi ya Taifa Arusha waliweza kumkamata Bwana Elias Sifael wa Leguruki Nkoasenga kwa kukutwa na silaha aina ya Shotgun namba C 139415 inayoaminika kutumika kwa ujangili.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa Tanzania
16/07/2013
0 comments:
Post a Comment