Wagosi wa kaya, Wagosi wa ndima, Coastal Unioni ya jijini Tanga, “Waja leo waondoka leo” jioni ya leo wameshuka dimbani kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wakusanyaji wa mapato wa nchini Uganda, klabu ya URA, katika uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani humo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Bao hilo pekee limetiwa nyavuni na mshambuliaji mpya aliyesajiliwa kutoka kikosi cha Polisi Morogoro, keneth Masumbuko, aliyemalizia pasi nzuri ya Seleman Uhuru Mwambungu baada ya kuwatoka mabeki wa URA katika dakika ya 70.
Wagosi wa Kaya wamefanya kitu ambacho mashabiki wa soka walikuwa wanahitaji baada ya URA kuifunga Simba uwanja wa taifa jumamosi ya wiki iliyopita na kutoka sare ya 2-2 na Yanga jumapili, lakini leo wamesalimu amri baada ya kukubali kichapo.
Akizungumza na MATUKIO DUNIANI Kocha wa klabu hiyo, Mzanzibar, Hemed Morroco amesema mchezo ulikuwa mzuri na kilikuwa kipimo sahihi kwa kikosi chake.
“Ilikuwa mechi nzuri sana kwetu, wachezaji wameonesha kiwango kizuri ingawa hatujakaa kambini muda mrefu. Lakini ninachokifanya kwa sasa nikutafuta kikosi cha kushindana mara ligi kuu itakapoanza”. Alisema Morroco.
Morocco alisema kwa sasa changamoto kubwa ni kukisuka kikosi cha uhakika ambacho kitafika mbali sana, ingawa amekiri kuwa muda nao umekuwa tatizo kwani kuna mambo yanafanyika kwa haraka zaidi tofauti na mipango yake.
“Kwanza nawashukuru sana mashabiki wa Soka mkoani Tanga, wanaonesha sapoti kubwa sana kwetu. Mimi nafikiri tuna wajibu mkubwa wa kufanya vizuri ili kuwafakisha pale wanapotaka timu yao ifike, hivyo nitajitahidi na wasaidizi wangu kuhakikisha tunatwaa ubingwa au kushika nafasi tatu za juu”. Alisema
Wagosi wa kwanza wataanza harakati za kuusaka ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara mnamo Agosti 24 mwaka huu kwa kucheza mechi ya ugenini dhidi ya maafande wa JKT Oljoro katika dimba la kumbukumbu ya Sh. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
0 comments:
Post a Comment