Wagosi wa kaya, Wagosi wa ndima, Coastal Unioni ya jijini Tanga, “Waja leo waondoka leo” jioni ya leo wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wakusanyaji wa mapato wa nchini Uganda, klabu ya URA, katika uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani humo majira ya saa 10 kamili jioni.
Akizungumza na MATUKIO DUNAINI, Afisa habari wa klabu hiyo, Edo Kumwembe amesema maandalizi yamekamilika na wanajiandaa kupepetana na wakali hao wa Uganda ambao tayari wameshacheza na timu kubwa mbili, Simba na Yanga na kuzifundisha soka la uhakika.
“Si kila timu inaweza kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa, kuna klabu kubwa kama Mtibwa Sugar, Kagera, Ruvu Shooting, lakini hazijapata nafasi ya kucheza na URA, hivyo ni nafasi nzuri kwetu kujipima na timu ambayo imeonesha kiwango cha juu dhidi ya Simba na Yanga ndani ya muda wa saa ishirini na nne”. Alisema Kumwembe.
Kumwembe alisema URA ambao waliwafunga Simba mabao 2-1 jumamosi ya wiki iliyopita na kucheza mechi ya pili jumapili dhidi ya Yanga na kupata sare ya 2-2 wanaonesha ukomavu wao, hivyo kipimo hicho ni kizuri hasusani kwa wachezaji wapya waliowasajili wakiwemo Juma Nyosso na Haruna Moshi “Boban” kutoka Simba.
Afisa habari huyo ambaye pia na mchambuzi wa soka na mwandishi wa habari za michezo aliongeza kuwa kipindi hiki cha maaandalizi wachezaji wote wanaonesha kujituma zaidi kwa lengo kubwa la kupata namba katika kikosi cha kwanza cha kocha Hemed Morroco.
Kumwembe alisema kuwa kocha wa wagosi hao wa Kaya ana malengo ya kutwaa ubingwa msimu ujao au nafasi ya pili na tatu.
“Unajua sisi tunataka kufuata nyayo za Azam fc wenye dhamira ya dhati ya kupindua utawala wa Simba na Yanga, angalia kwa sasa jinsi ambavyo ushindani umeongezeka kuwania nafasi za juu, zamani zilikuwepo timu mbili tu, lakini kwa sasa wana lambalamba wameonesha uhai mkubwa sana, hivyo Morroco anasema lazima tuige mfano huo na tuungane nao kuzipindua klabu kongwe hapa nchini”. Alisema Kumwembe.
Wagosi wa kwanza wataanza harakati za kuusaka ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara mnamo Agosti 24 mwaka huu kwa kucheza mechi ya ugenini dhidi ya maafande wa JKT Oljoro katika dimba la kumbukumbu ya Sh. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
0 comments:
Post a Comment