Hiki ni moja ya kikosi cha Yanga msimu uliopita. Yanga ndio mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, hivyo wana kazi kubwa ya kuwakilisha Taifa medani ya kimataifa mwakani.Wakata miwa wa Mashamba ya Miwa yaliyopo Manungu Turiani Mkoani Morogoro, kesho wanashuka dimbani kukabiliana na Yanga uwanja wa Ally Hassan Mwinyi
………………..
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
“Siku zote mtu huvuna alichopanda”, hata katika soka huwa hesabu ziko wazi kuwa maandalizi mazuri ndio siri ya kupata mafanikio. Timu ikiandaliwa kwa umakini na kitaalamu, hakuna uchawi, na soka halina uchawi, Mafanikio yako wazi.
Kwa kutambua msemo huo hapo juu, kila klabu ya ligi kuu soka Tanzania bara inahangaika kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya msimu mpya wa 2013/2014 unaotarajiwa kuanza kushika kasi Agosti 24 mwaka huu.
Ndipo mtandao wa MATUKIO DUNAINI unanyosha rada zake mpaka maeneo ya Mashamba ya miwa ya Manungu Turiani, mji kasoro bahari, Morogoro, na kukumbana na Mtibwa Sugar, huku Habari ya huko ni kuwa leo hii wanaanza safari yao kuelekea mkoni Tabora ambapo hapo kesho katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi watapimana ubavu na mabingwa wa ligi kuu, klabu ya Yanga ya Dar es salaam.
Kocha wa Mtibwa Sugar Mecky Mexime amesema mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi, huku akiweka wazi kuwa Yanga ni kipimo kizuri kwao kwani wanacheza soka safi na wanawanandinga wazuri.
“Ndio kwanza tunajiandaa kwa ajili ya msimu ujao, kesho alhamisi tutacheza na Yanga mkoani Tabora na leo hii tunasafiri kuelekea huko. Ni mechi nzuri ya kupima uwezo wa wachezaji wangu ingawa tumeanza mazoezi siku chache zilizopita, kikubwa kwa sasa ni kuwa wachezaji wote wapo salama”. Alisema Mexime.
Mtibwa Sugar wamekuwa na upinzani mkubwa katika ligi kwa miaka mingi sasa na wamewahi kutwaa ubingwa huo, na msimu ujao Mexime amesema wanajiandaa kutwaa ubingwa ambao wameukosa kwa miaka mingi.
“Lengo letu ni kuchukua ubingwa msimu ujao, tunahitaji kuwa makini katika hili, lakini daima msingi wa mafanikio ni maandalizi mema”. Alisema Mexime.
Wakati Mtibwa wakisafiri kuelekea leo mjini Tabora, wapinzani wao Dar Young Africans tayari wamewasili huko tangia jana wakitokea kwa wasukuma wa mkoani Shinyanga ambapo walicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Uganda , KCC na kupigwa mabao 2-1.
Yanga ambao wametokea katika ziara ya kanda ya ziwa yenye lengo la kuwaonesha kombe mashabiki wao, wapo Tabora wakijiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa, na kesho kutwa Ijumaa wanarejea jijini Dar es salaam kuendelea na program zake nyingine.
Afisa habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema wachezaji wote wapo salama na wanawasubiri wakata miwa wa Manungu.
“Timu iko vizuri baada ya kutoka kanda ya ziwa, baada ya mchezo wa kesho tutajiandaa kurejea Dar, kikubwa kwa sasa mashabiki wetu wajue kuwa timu inaandaliwa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa na kimataifa”. Alisema Kizuguto.
Nao wekundu wa Msimbazi Simba wapo mkoani humo wakiendelea na mawindo yao ya ligi kuu wakiwa na timu mpya kwa asilimia kubwa.
0 comments:
Post a Comment