Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi, HANDENI
Serikali imeombwa kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo kwa kuwapa vifaa na uwezo wa kujiendeleza ili waweze kudumisha ajira isiyo rasmi na kujikwamua kimaisha.
Ombi hilo limetolewa na wanafunzi wa chuo cha ufundi cha Saweruo kilichopo Handeni mkoani Tanga wakati wa mahafali yao chuoni hapo.
Wahitimu hao walisema kama Serikali itasaidia kutoa vifaa vya ufundi na ruzuku kwa vijana waliojiajiri katika sekta hiyo ni wazi kuwa wataweza kujikwamua katika dimbwi la umaskini na kuondokana na utegemezi wa ajira zinazotangazwa na serikali ambazo mara nyingi zinakuwa na ushindani mkubwa na hazitoshi kwa wote.
Wamesema vyuo vya ufundi vimekuwa vikiwasadia vijana kuelekea kujitegemea kimaisha lakini mara nyingi wahitimu wamekuwa wakikwamishwa na kutokuwa na mitaji ya ununuzi wa vifaa vinavyowazesha kujiajiiri wenyewe katika sekta ya ufundi mijini na vijijini na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Naye Mgeni Rasmi katika Mahafali hayo Bi. Sharifa Abebe, ambae ni Diwani ya kata ya Kwamgwe wilayani Handeni, aliwaasa vijana kutochagua kazi na badala yake wajiunge katika vikundi na kubuni miradi itakayowakwamua kiuchumi kikiwemo kilimo na biashara mbalimbali.
Bi. Sharifa pia ametoa wito kwa walezi na wazazi wenye vijana waliomaliza vyuo vya ufundi kuwahimiza kutobweteka lakini pia kuwawezesha kwa vifaa vya kiufundi badala ya kuisubiri Serikali ambayo amesema ina mzigo mkubwa kitaifa.
“Niwaombe wazazi wenzangu, tuwashawishi vijana wetu wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari, kujiunga na vyuo vya ufundi ambavyo vipo katika maeneo mengi hapa nchini na wamalizapo wataweza kujiajiri wenyewe”. Aalisema Bi Abebe.
Wahitimu hao wamejifunza ufundi mbalimbali ukiwemo wa utengenezaji wa samani za majumbani na maofisini, ushoni na shughuli za mapambo katika kumbi za mikutano ama sherehe mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment