




Picha Zote na Frank Shija
………………..
Na Frank Shija – Maelezo
Serikali imesema kuwa kugundulika kwa gesi asilia yenye mita za ujazo takribani milioni 41.7 katika maeneo mbalimbali nchini kunafanya Tanzania kuingia katika taswira mpya katika kujenga uchumi wake.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospter Muhongo wakati wa hafla kutiliana saini mkataba wa makubaliano baina ya Tanesco na Kampuni ya China Power Investement kwa ajili ya mradi wa kuzalisha umeme kwa pamoja.
Profesa Muhongo amesema kuwa kuanzishwa kwa mradi huo wa uzalishaji wa umeme kwa ushirikiana na Kampuni kutaongeza thamani ya rasilimali ikiwemo gesi kwa kuwa uzalishaji wa umeme katika mradi huo utatumia gesi asilia.
Waziri huyo aliongeza kuwa umeme utakaozalishwa utatumika kwa matumizi ya ndani na ziada itauzwa nje ya nchi ili kuletea Taifa mapato na kukuza uchumi wake ambapo mapato hayo yatasaidia Serikali kujitegemea kwa kiasi kikubwa katika bajeti yake.
“Kupitia miradi ya uzalishaji umeme kama hii taifa letu sasa linaonyesha matumaini nahii ni dalili kwamba rasilimali tulizonazo zimeanza kutunufaisha sote, pindi mradi huu ukikamilika tutakuwa na uhakika wa umeme na maana yake uchumi wetu hautakuwa tegemezi tena”.Alisema Profes Muhongo.
Aidha Muhongo alisema kuwa hadi kufikia 2017 jumla megawati 1800 itakuwa imezalishwa kama umeme wa ziada, na hivyo kuweza kuuza nje ya nchi na kujipatia kipato.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa kupitia utaratibu wa ushirikishaji wa taasisi za umma na binafsi katika kutoa huduma za kijamii ndiyo ulioleta mafanikio ya kupata mradi huo ambao Tanesco na Kampuni ya China Power Investnment wameingia makubaliano ya kuzalisha umeme kwa pamoja.
Mhandisi Mramba aliongeza kuwa mradi wa uzalishaji umeme wa Kinyerezi namba III utazalisha umeme jumla ya mega wati 600 pindi utakapo kamilika.
Serikali kupitia Shirika lake la Usambazaji na Uzalishaji umeme (TANESCO) imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kufikia malengo yake katika kuhakikishia jamii inapata umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu.
0 comments:
Post a Comment