Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Wakati siku zinazidi kuyoyoma kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote kushuka dimbani, hekaheka za maandalizi zinazidi kushika kasi huku makocha wakihaha kusuka vikosi vya ushindani zaidi.
Maafande wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani wamesema wamekibadili kikosi chao kwa kusajili wachezaji wapya ambao watasaidia kutwaa ubingwa au kushika nafasi tatu za juu.
Akizungumza na MATUKIO DUNIANI, Kocha Mkuu wa klabu hiyo Charles Boniface Mkwasa “Masta” amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi huku akijivunia wachezaji wapya waliowasajili wakiwemo Stephano Mwasyika kutoka Yanga, Elias Maguli kutoka Prisons na wengine wengi.
Mkwasa alisema lengo lao ni kufanya vizuri msimu ujao endapo tu waamuzi wataacha kasumba ya kuzibeba baadhi ya timu.
“Msimu uliopita waamuzi walitukwamisha sana, walikuwa wanachezesha hovyo na kushindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka, endapo watabadilika na kuzingatia weledi wa taaluma yao, basi tutafika mbali”. Alisema Mkwasa.
Pia Mkwasa alibainisha kuwa msimu uliopita tatizo kubwa lilikuwa safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inakosa nafasi nyingi za kufunga, na ndio maana wamemsajili aliyekuwa mshambuliaji hatari wa Tanzania Prisons, Elias Maguli.
“Kazi yangu kubwa kwa sasa ni kunoa vijana wangu wa safu ya ushambuliaji, kila wakati naongea nao kuhusu umuhimu wa kutumia nafasi adimu wanazopata wawapo uwanjani. Unajua tatizo la wachezaji wetu ni kukosa umakini, lakini tunapambana nao ili kuwarekebisha na kufika pale tulipokusudia”. Alisema Mkwasa.
0 comments:
Post a Comment