



…………..
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Kilimanjaro.
Serikali kuu na Sereikali za mitaa zimetakiwa kuendelea kushirikiana ili kuwezesha uwepo wa ulinzi na usalama katika maeneo yote hapa nchini kwa kuimairisha na kuipa msukumo kampeni ya Baraka za utii wa sheria bila shuruti inayosimamiwa na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (PCT).
Hayo yalisemwa jana na Naibu waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Baraka za utii wa sheria bila shuruti uliofanyika katika viwanja vya mashujaa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi.
Mwanri alisema suala la ulinzi limewekwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Jeshi la Polisi lakini wananchi wapo katika serikali za mitaa ambazo zipo chini ya TAMISEMI hivyo wakishirikiana vyema wataweza kuutokomeza uhalifu kwa uratibu mkubwa wa kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya mkoa hadi katika mitaa.
Alisema jambo linalofanywa na PCT ni kubwa kwa sababu wanawahubiri watu kuacha kujichukulia sheria mkononi na kufuata maandiko ya Mungu na kuachana na vitendo viovu hali ambayo itasaidia kupunguza gharama katika kuwashurutisha watu kutii sheria.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika uzinduzi huo IGP Said Mwema ambaye aliwakilishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro ACP Robert Boaz alisema ni vyema wananchi wakatii sheria bila shuruti ili kuongeza ustawi wa jamii na usalama hapa nchini.
Alisema kampeni hiyo inaliunganisha Jeshi la Polisi na Makanisa kwa kuwa wote wanafanya kazi moja ya kuhakikisha watu wanaacha kufanya maovu ambao makanisa na viongozi wa dini wanauita dhambi na kwa upande wa Jeshi la Polisi unaitwa uhalifu.
Naye Katibu Mkuu wa PCT Askofu David Mwasota alisema tangu kampeni hiyo ianzishwe imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa watenda maovu wamepungua na watu wanaotii sheria wameongezeka katika mikoa ambayo kampeni hiyo imeshazinduliwa ambapo wahalifu mbalimbali wamejisalimisha na wamekuwa watu wema.
Alisema wamekula njama njema na Jeshi la Polisi ya kuhakikisha kuwa watenda maovu wanaacha na mpaka hivi sasa kampeni hiyo imeshazinduliwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Kagera, Shinyanga, Dodoma, Katavi, Pwani na Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment