“Katika kila jambo Maandalizi ya mapema ni siri ya kufanikiwa, sisi tuna mipango mizuri zaidi kuhakikisha tunapata mafanikio msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara”. Maneno hayo yamesemwa na katibu mkuu wa maafande wa Jeshi la kujenga Taifa wenye makazi yao jijini Tanga, klabu ya Mgambo Shooting, Bwana Antony Mgaya.
Akizungumza na MATUKIO DUNIANI, Mgaya amesema walianza mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya tangu jumatatu ya wiki hii ambapo kazi kubwa ni kufanya usaili wa baadhi ya wachezaji wapya waliojitokeza katika mazoezi ya klabu hiyo ili kuangaliwa na makocha.
“Tangu tumemaliza mashindano ya majeshi kuadhimisha miaka 50 ya Jeshi la Kujenga Taifa, tumekuwa tukiendesha zoezi la kutafuta wachezaji ambao kocha ataridhika nao ili tuwasajili kwa ajili ya msimu mpya, wachezaji wengi hasusani waliocheza mashindano ya Majeshi wamejitokeza na kuna baadhi yao tumeshawakubali na sasa tunafanya nao mazungumzo ya kuwasajili”. Alisema Mgaya.

“Kwasasa tunafanya mazoezi tu, hatujaanza kambi rasmi, lakini jumatatu ya wiki ijayo tutaingia kambini tayari kwa ajili ya kujiwinda na msimu mpya” Alisema Mgaya.
Hata hivyo Mgaya alisema kuelekea msimu mpya, wamewaacha wachezaji 10 katika usajili wao, huku wachezaji 8 wakiwa ni maaskari ambao wamechaguliwa kwenda kujifunza kozi mbalimbali za kijeshi, wakati wawili ni raia waliomaliza mikataba yao.
Katibu huyo aliwataja wachezaji raia waliomaliza mikataba yao na benchi la ufundi kutangaza kutokuwa na mipango nao ni Juma Rajab na Musa Ngunda.
Wachezaji ambao ni maaskari wa jeshi na wameachwa katika usajili wao klabuni hapo ni Juma Lozana, Chande Hemed Mgoja, Omary Nassor Matiko, Juma Ali Mwinyimvua, Moka Shaban Dihimba, na Steven Kahaya.
“Tumeacha wachezaji 10, Kwa wale ambao ni maaskari hatujawaacha kwa sababu ya kushuka kiwango, lahasha!, wanaenda katika majukumu mengine ya kijeshi, watakapomaliza kama watataka kuendelea kuichezea timu yetu itakuwa ruksa kwao, lakini wataangaliwa kama bado wana kiwango kizuri”. Alisema Mgaya.
0 comments:
Post a Comment