DODOMA, Tanzania
MWANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi (VETA), mkoani Dodoma, Taliki Juma (22), amedaiwa kujiua kwa kujilipua kwa petroli kisa mapenzi.
Taarifa zinasema, kufuatia moto mkali uliotokana na petroli hiyo, mbali na mwanafunzi huyo aliyejitia mhanaga kwa mapenzi, watu wengine wanane waliokuwa karibu na moto huo nao walijeruhiwa vibaya.
Akithibitisha, leo Kamanda wa Polisi wa mkoa, David Misime, amesema tukio hilo lilitokea jana mida ya saa 12.30 jioni katika Kitongoji cha Machaka, Kata ya Nzughuni.
Kamanda alifafanua kwamba mapema mwanafunzi huyo alinunua lita tano za mafuta ya petroli katika kituo cha mafuta cha Nanenane na kisha kujilipua na kisha kwenda kujilipua akiwa katika saluni ya Irene Mapunda ambaye inasadikiwa alikuwa mpenzi wake.
Alisema, mwanzoni watu waliokuwa karibu naye walijaribu kumsihi asijilipue lakini hawakufanikiwa, kwani aliwasha kibiriti ndani ya saluni hiyo na kusababisha moto mkubwa kulipuka ambao uliwaunguza wengine waliokuwa karibu naye pamoja na mali zote zilizokuwa ndani ya Saluni hiyo kuteketea.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hili,” ilieleza taarifa ya Kamanda wa Polisi.
Taarifa iliwataja waliojerihiwa kuwa ni Mugina Hessein (32), Benson Mushi (11) Japhet Japhet (18), Meshack John (18), Swaibu Kassim (20),Ester Silau (30), Shaban Pili (20) na Fedrick Gabriel (21) ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na tathimini ya hasara iliyosababishwa na moto huo bado haijafahamika.
HABARI NA PICHA KWA HISANI YA NKOMOROBLOG
0 comments:
Post a Comment