Na Baraka Mpenja
Wakata miwa wa Kagera Sugar “Wanankulukumbi” wenye makazi yao katika dimba la Kaitaba mkoani Kagera wanaendelea kujifua vilivyo kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza Agosti 24 mwaka huu ambapo wao wataanza ugenini uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuvaana na wapya wa ligi hiyo, klabu ya Mbeya City.
Akizungumza na mtandao wa MATUKIO DUNIANI kwa njia ya simu kutoka Kaitaba, Afisa habari wa klabu hiyo, Hussein Mohamed amesema mazoezi yanaendelea kwa kasi kubwa chini ya kocha mpya lakini mwenyeji wa kazi hiyo klabuni hapo kwani alikuwepo kabla ya Kibadeni, namzungumzia Mganda Jackson Mayanja.
“Baada ya kumaliza usajili wetu, sasa timu ipo kambini kujiandaa na michuano ya ligi kuu. Lakini kikubwa kikosi chetu hakikubadilika sana, tumeongeza wachezaji kadhaa ili kuziba nafasi zilizobaki wazi baada ya wachezaji wetu kuondoka, pia kuziba mapungufu yaliyokuwepo msimu uliopita”. Alisema Hussein.
Hussein aliwataja wachezaji waliosajiliwa kuwa ni Antony Agaton kutoka Polisi moro, Peter Mutabazi (Toto African), Suleiman Kibuta (Toto African), Rashid Loshwa (Villa Squad), Adam Kingwande (Africa Lyon), Godfrey Wambura (Abajalo) na Mganda Hamis Kitagenda (URA).
Afisa habari huyo aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea kujifua mkoani Kagera, lakini mapema mwezi ujao watasafiri kuelekea Kisumu Kenya ambako wamealikwa kushiriki michuano ya Viwanda vya Sukari.
“Tutaenda kushiriki mashindano ya Viwanda vya sukari Kisumu Kenya, tumeshapata barua ya kwanza ya mualiko, lakini Mtibwa Sugar nao watakuwepo. Tunachosubiri kwa sasa ni barua ya pili itakayoonesha ratiba yote na taratibu za mashindano. Halafu nasikia hata Simba walialikwa ingawa mpaka sasa wana suasua kuthibitisha ushiriki wao”. Alisema Hussein.
Hussein alisema kikubwa ambacho kocha wao mpya, Jackson Mayanja anasema ni kuhakikisha wanapata nafasi nzuri zaidi ya msimu uliopita ambapo waliishia nafasi ya nne katika msimamo wakiongozwa na kocha mkongwe ambaye kwa sasa yupo na wekundu wa Msimba, Simba, Abdallah Kibadeni “King Mputa”.
“Mayanja amekubaliana na kikosi chake na kuahidi kufanya vizuri msimu ujao. Kocha huyu sio mgeni kabisa, alikuwepo kabla ya kuja kwa Kibadeni, alifanya kazi kubwa na baadaye aliondoka kwenda kwao kutokana na kupewa majukumu ya kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda, lakini sasa amerudi kazini kwake na atatuongoza kwa uzuri”. Alisema Hussein.
Msimu uliopita wa ligi kuu soka Tanzania bara uliomalizika mei 18, Kagera Sugar ilitajwa kuwa mojawapo ya timu zilioonesha ushindani wa hali ya juu,huku kocha wake mzee Kibadeni akipata tuzo ya kocha bora wa msimu
0 comments:
Post a Comment