Shabiki namba moja wa michezo nchini, Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alikutana na wachezaji uwanja wa ndege wa Mwanza na kuwatia moyo na kuwatakia kila la kheri.
………………….
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Homa ya pambano la kukata na shoka kuwania kufuzu fainali za tatu za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazopigwa mwakani nchini Afrika kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars dhidi ya Uganda (The Cranes) inazidi kupanda jijini Kampala huku wachezaji wa Stars wakiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi mbele ya wapinzani wao.
Mechi hiyo itapigwa kesho katika dimba la taifa la Nelson Mandela, lililopo Namboole , nje kidogo ya jiji la Kampala majira ya saa kumi kamili jioni kwa saa za afrika mashariki.
Afisa habari wa shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, Boniface Wambura Mgoyo alikaririwa na mtanadao huu akisema Kocha wa Stars Kim Poulsen tayari ameshawajenga kisaikolojia wachezaji wake, hivyo katika mchezo wa kesho wanaweza kupata matokeo mazuri na kufuzu fainali za CHAN.
Wambura alisema Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho leo (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.
Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.
Kwa upande wake Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.
Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.
Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
0 comments:
Post a Comment