Moto mkubwa ulioanza katika Mlima Kilimanjaro tangu siku ya Jumapili tarehe 7.7.2013
umeendelea kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa bila kuathiri shughuli za utalii katika Hifadhi ya Kilimanjaro.
Hadi kufikia leo tarehe 9.7.2013 moto umedhibitiwa kwa kiwango cha asilimia 75 na dalili zinaonyesha kuwa katika kipindi kifupi kijacho utaweza kudhibitiwa wote.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama ametoa agizo kwa wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro kushiriki operesheni maalum ya kuzima moto huo kwa kutoa askari mgambo watakaoshirikiana na TANAPA katika kuzima moto.
Hifadhi ya Kilimanjaro imeweka kambi mbili maalum kwa ajili ya kuhudumia wanaoshiriki zoezi la kuzima moto moja ikiwa katika eneo la Nanjara wilayani Rombo ambako ndipo ulipo sehemu kubwa ya moto na kambi ya pili ipo katika eneo la Marangu kwa ajili ya kuhudumia eneo la Kilema Juu.
Shughuli za Utalii katika Mlima Kilimanjaro zinaendelea kama kawaida na hakuna watalii wowote walioathirika na moto huu hasa kwa kuwa njia zote muhimu za Marangu, Mweka, Machame, Umbwe, Lemosho na Rongai zinazotumika kwa ajili ya kupandisha watalii mlimani na zile za kushukia hazijaathiriwa na moto.
TANAPA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea na juhudi za kutafuta waliohusika na uharibifu huu na mara zoezi la kuzima moto litakapokamilika taarifa ya tathmini ya madhara ya moto itaweza kufanywa.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa Tanzania
09.07.2013
0 comments:
Post a Comment