Na Baraka Mpenja
Wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani mkoani Morogoro,
mji kasoro bahari, Mtibwa Sugar, wanatarajia kuanza zoezi la usajili mapema
mwezi ujao, huku akibainisha kuwa wamechelewa kufanya hivyo ili kuwavutia kasi
Simba na Yanga wenye tabia ya kuwachukuliwa wachezaji wao.
“Mambo mazuri hayahitaji haraka, timu kubwa zina tabia ya
kutuchukulia wachezaji, lakini mwezi ujao tuanza kazi rasmi ya kutafuta bunduki
za kuwashambulia katika msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara”. Alisema Mexime.
Akiongea na Mtandao wa MATUKIO DUNIANI,
Kocha mkuu wa klabu hiyo Mecky Mexime ambaye aliibuka shujaa baada ya
kuchaguliwa kuwa kocha bora wa ligi kuu msimu uliopita na chama cha wachezaji
wa soka Tanzania (SPUTANZA), alisema usajili wao utaanza kwa kutafuta mlinzi
mahiri wa kushoto baada ya “Baba ubaya”, Issa Rashid kutimkia kwa wekundu wa
msimbazi Simba kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Mexime alisema katika usajili wao, kamwe hawatafanya makosa
ya kuwafanya wajutie, kwani wana malengo makubwa ya kufanya vizuri msimu ujao
na kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara au kushika nafasi tatu za juu.
“Uwezo wetu watu wanaojua sana, sasa tutaongeza mara dufu
kwa kusajili wachezaji wazuri zaidi, nia yetu ni kuwasumbua wakongwe wa soka la
Tanzania ambao kila siku wanapigana vikumbo kwa kusajili wagalasa kutoka nje ya
nchi, wakifika hapa wanakomba pesa zao bila kazi yoyote”. Alisema Mexime.
Wakati Mexime akisema hawajaanza usajili, taarifa za ndani
kutoka klabuni hapo zinaeleza kuwa tayari wameshamsajili mlinzi wa maafande wa
JKT Oljoro ya jijini Arusha, Salim Mbonde na ameshasaini dili za mkataba wa
miaka miwili.
Kocha huyo mwenye historia ya kuzikataa Simba na Yanga
katika enzi zake za soka mpaka anastaafu, alisema ni muhimu kwa mashabiki wao
kuwa na utulivu kipindi hiki cha usajili wakati benchi la ufundi likiendelea
kutafuta mashine mpya za ligi kuu msimu ujao.
0 comments:
Post a Comment