Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga,
ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF,
alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali
imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya
klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine
muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa
tamko.
“Masuala
ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali
itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama
ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu
la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika
Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama
kutoka nchi mwenyeji.
“Kama
tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi
moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali
hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga
alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika
dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi
mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.
Alisema
wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa
Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa
dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka
uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia
baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo
nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa
usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama
wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi
anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,”
alisema Tenga.
“Lakini
napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa
mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas
Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua
viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.
Alisema
watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu
Darfur.
“Mhe.
Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya
usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda
Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa
maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu
hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la
Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa
mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini
ndipo tuziite timu.”
Alifafanua
kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba
chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji
gani.
“Sasa
kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini
na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike
kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,”
alisema.
“Sasa
ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu
ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”
0 comments:
Post a Comment