Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo
na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake
ya kesho (Juni 8 mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini Marrakech.
Stars,
ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali
ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi
moja, inacheza na Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika Marrakech
baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza
iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Machi.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa
tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa
Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa
kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.
“Katika
kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji
yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi
uliofanyika kwenye ofisi za TFF.
“Lakini
katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi
kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji;
kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia
tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata
kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).
“Posho
za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo
wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu.
Watu wanasema usione vinaelea….”
Tenga
alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza kuzaa matunda na timu
inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya muda mrefu.
“Sasa
tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda
Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona
kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.
Rais
huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu
Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia
kuongeza hamasa kwenye timu.
Naye
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake
itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande
hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.
Katika
mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilikabidhi
fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco
kuishangilia timu.
Ofisa
Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema tayari fulana 250
zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa
kusafirishwa jana.
0 comments:
Post a Comment