Na Baraka Mpenja
Katika
harakati za kuhakikisha wanarejea kucheza ligi kuu soka Tanzania bara
msimu wa 2014/2015, wapiga kwata wa Polisi Morogoro wanaendelea na zoezi
la kusaka wachezaji wapya kwa ajili ya kuziba nafasi zilizoachwa wazi
kufuatia wachezaji kadhaa kuihama klabu hiyo na wengine kumaliza
mikataba yao.
Akizungumza na MATUKIO DUNIANI
kutoka Morogoro, Afisa habari wa Polisi Moro, Clemence Banzo amesema
kuwa klabu hiyo inaendelea na mazoezi ya kusaka vipaji vipya ambapo
wachezaji kutoka maeneo mbalimbali wameitwa kufanya usaili na
watakaoonekana wanafaa watasajiliwa ili kuungana na wenzao wakongwe.
“Muda
si mrefu tumetoka mazoezini, unajua kushuka daraja kumetupotezea ari
sana, lakini kwa kujua kuwa tunahitaji kurudi ligi kuu ndani ya mwaka
mmoja tumeanza kuziba nafasi zilizowazi kwa kuwafanyia usaili wachezaji
wapya, naamini tutafanya vizuri”. Alisema Banzo.
Afisa
habari huyo alisisitiza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kocha wao Rishard
Adolf aliyerithi mikoba ya kocha John Simkoko kipindi cha mzunguko wa
pili wa ligi kuu msimu uliopita na kupata pointi 21, uongozi wa klabu
umeamua kumpa mkataba wa miaka miwili ili airudishe ligi kuu.
“Adolf
ni mwalimu mzuri, alitusaidia sana ingawa tulishuka daraja, tumempa
mkataba mwingine, tunaamini ndani ya mwaka mmoja tunarejea ligi kuu
bara”. Alisema Banzo.
Banzo
aliongeza kuwa katika mazoezi hayo, kikubwa ambacho Adolf anakihitaji
ni wachezaji kucheza kwa kujituma na kutambua kuwa soka ni ajira yao.
Aidha
afisa habari huyo alisisitiza kuwa Adolf ni mtu anayependa nidhamu kwa
wachezaji na amewataka kucheza soka kwa kuisaidia timu hiyo.
“Mazoezi yamenoga sana na mwalimu wetu anatupa matumaini makubwa sana”. Alisema Banzo.
Pia
Banzo alisema hapo kesho kama mambo yatakwenda vizuri, wanatarajia
kucheza mechi ya kirafiiki dhidi ya wekundu wa Msimbazi Simba katika
dimba la Jamhuri mkoani Morogoro.
“Tunawasiliana
na Simba ili tupate mechi ya kirafiki na kupima uwezo kikosi chetu,
tuombe mungu ili mambo yaende sawa. Kama mipango itanyooka, basi Mnyama
atakuwepo hapa Morogoro kesho”. Alisema Banzo.
0 comments:
Post a Comment