Na Baraka Mpenja
Kocha
wa wagosi wa kaya wagosi wa ndima wa jijini Tanga “waja leo waondoka
leo” Coastal Union, Hemed Morroco ametamba kufanya vizuri msimu ujao wa
ligi kuu Tanzania bara, huku akisema tuhuma za utovu wa nidhamu dhidi ya
Haruna Moshi ‘Boban’, Juma Nyosso na Amir Maftah, haziwazuii kuwasajili
kwenye kikosi chao kwa msimu ujao.
Morocco
amesema watafanya maandalizi ya nguvu ili kuleta ushindani mkubwa zaidi
katika Ligi Kuu iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24.
“Tunaanza
mazoezi mapema mwezi ujao, nina imani nitaanza kwa kuyafanyia
marekebisho baadhi ya makosa ambayo yalijitokeza msimu uliopita japokuwa
nina nyota wapya katika kikosi changu,” alisema Morroco.
Akisisitiza
suala la utovu wa nidhamu kwa wachezaji Bobab, Nyoso na Maftah, Morroco
alisema hilo halimpi shida kwa sababu kwanza anataka kujionea mwenyewe
utovu huo wa nidhamu na zaidi ya hapo, kila kocha ana falsafa zake
kiufundishaji, hivyo atajitahidi kwenda nao vizuri kwani ni nyota wenye
uwezo mkubwa.
Morroco
alisema utovu wa nidhamu ni suala pana, hivyo licha ya kuwepo kwa
tuhuma hizo dhidi yao, haoni kama ni sababu ya kutowasajili.
“Kila
kocha ana falsafa yake, siwezi kumsemea Liewig, nataka nijionee
mwenyewe utovu wao wa nidhamu, sio kuwaacha tu kwa kusikia kwa watu,”
alisema Morroco na kuongeza anaamini watakuwa wachezaji wazuri.
Pia
kocha huyo aliyeiongoza klabu hiyo msimu uliopita na kumaliza katika
nafasi ya sita, aliongeza kuwa mashabiki wa kandanda mkoani Tanga wasiwe
na shaka kwani kikosi chake kimesheheni majembe ya ukweli.
“Ni
wachezaji bora sana, nataka kushindana na kuzipiku klabu zilizokuwa juu
yetu msimu uliopita, mazoezi yatakuwa maalumu kujiandaa kutwaa ubingwa
wa ligi kuu, kikubwa mashabiki watupe sapoti kubwa”. Alisema Morocco.
0 comments:
Post a Comment