Na Baraka Mpenja
Wakati
siku zinazidi kuyoyoma kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars
kukabiliana na Simba wa milima ya Atlas mnamo juni 8 mwaka huu nchini
Morroco, makocha mbalimbali wa soka wazidi kutoa tathmini yao kuhusiana
na mchezo huo, huku wengi wakiamini stars inaweza kupata matokeo mazuri
ugenini.
Kocha
mkuu wa maafande wa Ruvu Shooting wa mkoani Pwani na kocha wa zamani wa
timu ya tifa ya wanawake “Twiga Stars”, Charles Boniface Mkwasa
“Masta” ameimabia MATUKIO DUNIANI kuwa matokeo ya jana usiku ambapo
Stars ilitoka suluhu ya bila kufungana na Sudan hayana athari yoyote kwa
kikosi cha Kim Paulsen ila yamempa nafasi ya kuona makosa ya timu yake.
Mkwasa
amesema mara zote makocha wanatumia mechi za kirafiki kuangalia uwezo
wa vikosi vyao, na kama timu imeshinda mechi ya kirafiki inakuwa ngumu
kuona makosa kirahisi, lakini inapopoteza mchezo inakuwa nzuri zaidi
kugundua makosa.
Mkwasa
alisema Sudan kwa sasa hawatishi sana, lakini mpira wao unafanana na wa
Tanzania, mara nyingi Stars inakutana nao katika michauno ya kombe la
CECAFA, hivyo matokeo ya jana ni ya kawaida.
“Malengo
ya Stars sio kushinda mechi za kirafiki bali kuna mechi za mashindano
ambazo mwalimu anazipa uzito mkubwa, kushindwa kuwafunga Sudan sio
tatizo, kikubwa vijana wajengwe kuelekea mchezo wa juni 8 dhidi ya
Morroco”. Alisema Mkwasa.
Kocha
huyo aliongeza kuwa kuna wachezaji wawili wa safu ya ushambuliaji ambao
walikosa mechi hiyo kutoka TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu , na watakapoongezeka kule Morroco timu itakuwa na nguvu zaidi
kwani vijana hao wana uwezo mkubwa kwa sasa.
“Binafsi
Morroco nawaheshimu sana, tuliwafunga nyumbani mabao 3-1, sio sababu ya
kuwadharau, kinachotakiwa ni wachezaji wetu kupigania taifa na
kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kuendelea kujipatia matumaini
makubwa ya kucheza fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil”.
Alisema Mkwasa.
Mbali
na Mkwasa, aliyekuwa kocha wa JKT Oljojoro na mchezaji wa zamani wa
Taifa stars, Mbwana Makata amesema kuwa timu inapopoteza mchezo wa
kirafiki wakati ikijiandaa na mechi ya mashindano ni vizuri zaidi kuliko
kupata matokeo ya ushindi ambao yanaficha mabaya zaidi.
“Ukishinda
unajiona unaweza na kubweteka, matokeo ya jana nimeyapenda, toka mwanzo
nilikuwa naomba stars wasishinde ili mwalimu ajue cha kufanya, suluhu
ya jana nadhani itawasaidia kupata nguvu mpya na kujiona wanahitaji
kujituma”. Alisema Makata.
Makata
alisisitiza kuwa kikosi cha stars kina morali kubwa, udhamini mnono,
wachezaji vijana wenye nguvu na kasi kubwa, hivyo kuwabania Morroco na
kuwatandika wakiwa kwao inawezekana kutegemeana na mazingira halisi ya
huko.
“Nina
imani na vijana wetu, sina shaka na kocha wetu, vijana wana mazingira
mazuri sana, kila kitu kipo, morali ni kubwa tofauti na miaka ya nyuma,
wamefanya vizuri mechi za kirafiki na kuzifunga timu kubwa wakiwemo
Zambia na Cameroon, hii ni motisha tosha kabisa, kila la heri vijana
wetu”. Alisema Makata.
Naye
aliyekuwa kocha wa African Sports ya Tanga na sasa mjumbe wa kamati ya
ufundi ya wekundu wa Msimbazi Simba, Mwalimu John Wiliam maarufu kwa
jina la “Del Piero” amesema ushindi katika mchezo wa Morroco uko pale
pale kutokana na kocha wa Stars kujua soka la wapinzani wake.
“Kim
alienda Afrika kusini kuwatazama Morroco, wengi hawakujua maana ya ile
ishu, hakika ilimpa uwezo mkubwa wa kuwajua wapinzania wake, madhaifu
yao na makali yao, na ndio maana mechi ya kwanza aliwafunga kirahisi,
sidhani kama wamebadilika sana, kikubwa ni vijana kuzingatia maelekezo
ya mwalimu”. Alisema Piero.
Safari
ya Brazil ipo na lazima Tanzania ifike huko, licha ya kupambana na timu
kubwa wakiwemo Tembo wa Pwani ya magharibi ya Afrika,Ivory Coast,
Gambia na waarabu wa Morocco.
Kila la heri taifa stars, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Taifa Stars.
0 comments:
Post a Comment