WAZIRI
MKUU Mh. Mizengo Pinda amezindua mradi maalum wa vitabu vya elektroniki
vya masomo mbalimbali wenye thamani ya sh. milioni 100 ambao unalenga
kupunguza tatizo la ukosefu wa vitabu mashuleni na kuboresha elimu.
Akizungumza
na mamia ya wakazi wa vijiji vya Nganana na Nambala wilayani Arumeru
mwishoni mwa wiki kwenye uzinduzi wa mradi wa vitabu vya kieletroniki
(Nganana E-Reader Project), Waziri Mkuu alihimiza utunzaji wa vitabu
hivyo.
“Nimeambiwa
kuwa vifaa hivi vina uwezo wa kubeba vitabu 2,000 kila kimoja, na hivyo
kutumika kama ‘maktaba za mkononi za vitabu-elektroniki’. Hapa mmepata
vifaa vya vitabu-eletroniki 300 na kila kimoja kimewekewa vitabu 100
ndani yake. Sasa ni wapi hapa nchini unaweza kukuta shule au taasisi
ambayo inamwezesha kila mwanafunzi kuwa na vitabu 100 yeye peke yake,”
alihoji Waziri Mkuu na kushangiliwa.
Waziri
Mkuu alisema mradi huo utawasaidia watoto wa shule za msingi za Nganana
na Nambala kuongeza ujuzi na kukuza upeo wao wa kuelewa mambo.
“Ninawapongeza waliobuni mradi huu kwa sababu vitabu-elektroniki
havizeeki wala kuchanika, tofauti na vitabu vya makaratasi, hebu
kiangalie ni wakati gani kitu kama hiki kitachakaa,” alihoji.
Alimshukuru
Mkurugenzi wa Taasisi wa World Reader ya Marekani, Bw. David Risher kwa
kuendesha harambaee huko kwao iliyochangia kupatikana kwa
vitabu-elekroniki 200 vya ziada na kuiwezesha Taasisis ya Nelson Mandela
kupata vifaa 300 wakati uwezo wao ulikuwa ni kununua vifaa 100 tu. Pia
aliushukuru uongozi wa Taasisi ya Nelson Mandela kuwa kubuni mradi huo.
Waziri
Mkuu alikabidhi vyeti maalum vya uzinduzi kwa walimu wakuu wa shule za
msingi za Nganana na Nambala, Bw. Samuel Pallangyo na Bw. Joseph Mushi.
Akizungumzia
taasisi yake ya World Reader, Bw. Risher alisema alisukumwa kuanzisha
utunzaji wa vitabu kwa njia ya elektroniki baada ya kutembelea maktaba
moja na kukuta imewekewa kufuli kubwa kwa sababu ilikuwa imejaa vitabu
viliyopitwa na wakati.
Alisema
tangu utotoni, mama yake alizoea kumuacha maktaba wakati yeye (mama)
akifanya shughuli zake na kisha kumpitia warudi nyumbani. “Jambo hili
lilinifanya nijenge mazoea ya kupenda kusoma vitabu,” alisema.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzindia mradi huo, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa alisema Taasisi ya Sayansi
na Teknolojia ya Nelson Mandela katika jitihada zake za kushughulikia
masuala yanayoikabili jamii, imebuni mradi huo unaolenga kutumia TEHAMA
kuamsha na kuchochea usomaji vitabu kwa kutumia kifaa kinacholingana kwa
jirani na simu za mkononi.
Naye
Makamu Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Prof. Burton Mwanilwa akitoa
maelezo ya mradi huo alisema chimbuko lake limetokana na nia ya Chuo
cha Nelson Mandela kujaribu kutatua changamoto za elimu zinazoikabili
jamii. “Chuo kinategemea wanataaluma na wanafunzi wake watoke shule za
msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na hizi za Nambala na Nganana ambazo
ziko jirani kabisa na chuo chetu,” alisema.
Alisema
walipofanya tathmini ya mahitaji, walibaini kuwa wanahitaji E-readers
100 zitakazogharimu dola za marekani 22,000 (zaidi ya sh. milioni 33)
lakini kwa vile Chuo hakikuwa na bajeti ya mradi huo, waliamua
kuchangisha fedha kutoka kwa wanajumuiya ya chuo, wazazi, wanafunzi na
wadau wa mkoa wa Arusha.
“Baada
ya kuiona nia yetu ya kulipia E-Readers 100, taasisi ya World Reader
ilishawishika kuchangisha fedha huko Marekani na kutuwezesha kuapata
E-Readres 200 zaidi na kufanya idadi ifikie E-Readers 300,” alisema.
Alisema
walimu 29 walipatiwa mafunzo ya siku mbili na jinsi ya kutumia vifaa
hivyo na tayari walikwishaanza kutoa mafunzo ya awali kwa wanafunzi wao.
0 comments:
Post a Comment