Mkuu
wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, amewataka Wazazi wa Wanafunzi
hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao Shuleni haraka kabla ya
kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi agizo hilo.

Wananchi na wazazi wakimsikiliza mkuu wa wilaya
Na E . Kamanga, Chunya
ZAIDI
ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika
Shule mbalimbali za Sekondari Wilayani Chunya Mkoani Mbeya wameshindwa
kuripoti shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiingiza katika
biashara za uchimbaji wa Madini na Uvuvi.
Kutokana
na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, amewataka
Wazazi wa Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao Shuleni
haraka kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi
agizo hilo.
Kinawiro
aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wananchi wa
Kitongoji cha Majengo, kata ya Sangambi Wilayani humo baada ya kupokea
taarifa kutoka kwa Afisa elimu wa Wilaya kuhusu kukithiri kwa utoro wa
wanafunzi shuleni, hivyo kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo
yake ya kufuta ujinga miongoni mwa wananchi.
Alisema
Wilaya ya Chunya inakabiliwa na Wimbi kubwa la wafugaji wenye tabia ya
kuhamahama jambo ambalo husababisha kuwakatisha masomo wanafunzi ili
hali wengine wakijikita kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi
katika Ziwa Rukwa.
Alisema
kufikia mwishoni mwa mwezi huu mzazi yeyote ambaye hatampeleka mwanae
Shule bila kujali kisingizio cha aina yoyote atakamatwa na kufikishwa
mahakamani kujibu mashtaka ya kumwachisha masomo mwanafunzi na kumpatia
ajira kinyume cha Sheria.
Mkuu
huyo wa Wilaya alisema Idadi ya watoto 500 ni kubwa sana hivyo hali
hiyo ikiachwa itazalisha wajinga wengi jambo ambalo litakuwa mzigo kwa
taifa kutokana na wengine kuwa majambazi baada ya kukosa fedha kutokana
na ajira walizojiingiza katika umri mdogo na kukwamisha juhudi za
Serikali za kujenga Shule kila kata.
Kinawiro
alisema Wilaya ya Chunya kitaaluma inafanya Vizuri katika ngazi ya Mkoa
ukilinganisha na Wilaya zingine, hivyo hayuko tayari kuona sifa hiyo
inapotea kutokana na wazazi wachache kuzembea na kutokujua umuhimu wa
kumsomesha mtoto.
Mkuu
huyo wa wilaya alisisitiza kuwa Halmashauri inaunga mkono juhudi za
Serikali kwa kuimarisha ujenzi wa Mabweni ili kuhakikisha watoto wa kike
hawakatizwi masomo kutokana na mimba zisizotarajiwa.
Wakati
huo huo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wafugaji wote waliohamia Wilayani
Chunya kinyume cha Sheria kuondoka mara moja na atakaye kaidi agizo
hilo atakumbana na operesheni kubwa ya kuwaondoa kwa nguvu ambapo kwa
sasa wanafanya doria kwa kutumia ndege maalumu kuwabaini wahamiaji hao.
Alisema
zoezi hilo litafanyika hivi karibuni baada ya kumaliza kuwabaini
wafugaji waliovamia misitu na sehemu za hifadhi ambapo wanaharibu
mazingira kutokana na idadi kubwa ya mifugo.
Hivi
karibuni kulifanyika zoezi la kuwaondoa wafugaji waliovamia msitu wa
hifadhi wa kijiji cha Mbangala ambapo jumla ya mifugo 1000 ilikutwa
msituni humo, lakini zoezi hilo liliingiliwa na hitilafu baada ya
wafugaji hao jamii ya Wamang’ati kuwashambulia kwa mishale na mikuki
maofisa pamoja na Askari wa Jeshi la Polisi waliokimbia kunusuru maisha
yao.
(Picha kwa Hisani ya blog ya Mbeya Yetu)
0 comments:
Post a Comment