Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameitakaSerikali kuharakisha kuulet
a
bungeni Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari ili
kuhakikisha waandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata
maadili na misingi ya taaluma hiyo.
Wakichangia
hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
nyakati tofauti, wabunge hao waliipongeza wizara hiyo kwa kuridhia
Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari kwa kuwa itasaidia kuikuza na
kuiimarisha taaluma ya habari nchini.
Akichangia
hotuba hiyo mbunge wa viti Maalum (CCM) Esther Bulaya alisema wakati
umefika kwa waandishi wa habari nchini kuandika habari kwa kuzingatia
maadili ya taaluma hiyo ikiwa ni pamoja na kuandika habari zilizofanyiwa
utafiti wa kina na zinazohusisha pande mbili za chanzo cha habari.
Mhe.
Bulaya amewataka waandishi wa habari wasitumie vibaya uhuru wa habari
kwa kutoa habari zinazoshabikia vyama vya siasa na zenye kuleta chuki
zitakazowafanya vijana kujenga taifa la visasi. Aliongeza kuwa taifa ni
zaidi ya vyama vya siasa.
Naye
mbunge wa Kondoa Kusini, Mhe. Juma Nkamia alisema kupatikana kwa sheria
ya kusimamia vyombo vya habari kutasaidia kuondokana na tatizo lililopo
sasa la kuwa na waandishi wa habari wengi wasiokuwa na sifa maarufu
kama ‘makanjanja’.
Akizungumzia
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Nkamia aliitaka serikali kupitia
wizara ya habari kuhakikisha inafanya kila liwezekanalo kuyamalizia
majengo yaliyopo Mikocheni ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa majengo hayo yaliwekwa jiwe la msingi na Rais wa awamu ya
pili Mzee Ali Hassan Mwinyi lakini mpaka sasa ni Serikali ya awamu ya
nne na majengo hayo hayajakamilika.
Mhe.
Nkamia pia aliitaka serikali kuiongezea bajeti TBC ili iweze kununua
vifaa vipya na vya kisasa vya kurushia matangazo kwa kuwa vifaa
vilivyopo vimechakaa. Aliongeza kuwa matangazo ya TBC hivi sasa hukatika
katika kutokana na tatizo hilo.
Akiwasilisha
hotuba ya Bajeti, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt.
Fenella Mukangara aliliambia bunge kuwa serikali imeridhia kutungwa kwa
Sheria ya Kusimamia Vyombo vya habari na muswada wa kutunga sheria hiyo
utawasilishwa bungeni hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment