Na Baraka Mpenj, Mbeya
Leo hii mtandao wa MATUKIO DUNIANI
imeshuhudia mazoezi makali ya klabu ya Tanzania Prisons “wajela jela”
katika dimba la CCM Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya chini ya kocha
wake mkuu Jumanne Chale ambaye amehangaika sana msimu huu kusalia ligi
kuu soka Tanzania bara na hatimaye amefanikisha ndoto yake hiyo.
Akizungumza
katika mazoezi hayo, Chale amesema hakika safari yao ilikuwa ngumu sana
msimu wa kwanza baada ya kuathiriwa na ajali mbaya ya gari na wachezaji
wao kujeruhiwa , lakini sasa timu imeunganika upya na inacheza soka
maridhawa.
“Tumefanikiwa
kubakia ligi kuu msimu huu, hakika ni jambo jema sana kwetu, hii ni
nafasi nzuri sana kujipanga upya msimu ujao ili kupambana kupata nafasi
za juu za msimamo na kuiwakalisha Tanzania katika michuano ya
kimataifa”. Alisema Chale.
Akizungumzia
mchezo wa funga pazia la ligi kuu msimu huu dhidi ya Kagera Sugar chini
ya kocha mkongwe kuliko wote ligi kuu kwa sasa, Abdallah Kibadeni “King
Mputa”, Chale alisema mchezo huo ni mgumu sana kutokana na uimara wa
wapinzania wao, lakini wanajiandaa kupata ushindi mwingine katika uwanja
wa nyumbani wa Sokoine jijini hapa.
Kwa
upande wake katibu mkuu wa Tanzania Prisons Sadick Jumbe alisema sasa
wanaanda majeshi ya kuwatafuna wakata miwa wa kaitaba mei 18 mwaka huu
na baada ya hapo watasubiri ripoti ya kocha wao ili kuifanyia kazi
katika dirisha la usajili.
“Uongozi
kwa kushirikiana na wadau wa soka jijini Mbeya tunajiandaa kusajili
kikosi kizuri cha ushindani msimu ujao, tutazingatia mapendekezo ya
mwalimu kwani yeye ndiye mtaalamu zaidi” alisema Jumbe.
Akizungumzia
maendeleo ya kikosi chao, Jumbe alisema amegundua kuwa timu inapotoka
daraja la kwanza na kucheza michuano ya ligi kuu, wachezaji wanahitaji
muda sana kuzoea, na ndio maana walihaha sana mzunguko wa kwanza.
“Hatukuwa
vizuri sana mzunguko wa kwanza, lakini sasa timu imeiva baada ya
wachezaji wetu kuzoea ushindani wa ligi kuu, na tunaamini msimu ujao
tutafanya vizuri zaidi”. Alisema Jumbe.
Baada
ya mazoezi ya leo hii asubuhi, wachezaji wamepumzika mpaka kesho ambapo
wataendelea kupasha moto misuli yao wakiwawinda Kagera Sugar.
0 comments:
Post a Comment