TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei
19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya kikao cha siku moja na wabunge
wanaotokana na CCM, kikao hicho kilifanyika mjini Dodoma ambapo pamoja
na viongozi wengine wa juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia na
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kikao
hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa CCM na viongozi wa CCM
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais na
mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kubadilishana uzoefu wa
namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi cha nusu ya
muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo
wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi
kilichobaki.
Kwahiyo
kwa kifupi lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa
ilani majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa
zaidi kwa kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya
CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha ilani na ahadi za CCM na
wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Hata
hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli
inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete kuwa
ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015
kufanya kampeni.
CCM
imesikitishwa na nukuu hiyo ya kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na
hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli
kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa au wanaojitaja kuwa na
nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na Urais
ulikuwepo na ulikuwa mkali.
Hata
hivyo hitimisho la kikao na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa
lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na uvunjifu huu wa
makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi zinakigawa
Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea
kuna kikundi cha watu wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka
anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha
Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya waandishi, uhuni huo haukubaliki.
CCM
ina kanuni na taratibu zake zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya
shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake
katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa.
Kanuni
hizo ni pamoja na kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika
vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM,
toleo la 2012.
Katika
Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33
inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa shughuli za uteuzi na
uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na
kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na wale wote
wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1).
“….wanachama wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina
yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao kinachohusika”.
(4).
“Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi
visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za
chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi
zilizowekwa”.
Ibara
hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni
wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM
kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za
uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na
kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na wabunge wa CCM
mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni
marufuku kwa mwanachama yeyote wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi
ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha na kuita wapiga
kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali
zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini
pia ni marufuku kwa viongozi na watendaji wa Chama kujihusisha na
kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia ya kugombea kupitia CCM
kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi na
watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.
Tunawataka wote wenye nia, viongozi na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
0 comments:
Post a Comment