Wachezaji
wa Yanga wakishangilia baada ya kupata goli la kwanza dhidi ya Simba.
Bao hilo lilifunga dakika ya tano ya kipindi cha kwanza baada ya mabeki
wa Simba kufanya makosa makubwa langoni mwao
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Kocha wa
klabu mpya ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao, Mbeya City kutoka
jijini Mbeya, Mwalimu Juma Mwambusi amesema kilichowagharimu wekundu wa
Msimbazi Simba katika kipute cha watani wa jadi na kufungwa mabao 2-0 ni
nafasi ya ulinzi kupwaya kwa msimu mzima wa ligi hiyo.
Mwambusi ameimabia MATUKIO DUNIANI
kuwa makocha wa Simba wamehangaika sana kutafuta wachezaji wa kucheza
nafasi ya ulinzi ili kuziba pengo la baadhi ya wachezaji waliotimka
Msimbazi akiwemo beki wa kati wa Yanga Kelvin Patrick Philip Yondan
aliyeihama Simba mwishoni mwa msimu wa mwaka jana.
Kocha huyo
aliyekuwepo uwanja wa taifa hapo jana kushuhudia mtanange huo uliovuta
hisia za mashabiki wengi nchini Tanzania amesisitiza kuwa bao la kwanza
la Yanga lilifungwa baada ya mabeki wa Simba kushindwa kukaba vizuri na
kujua wapi mpira utatua.
“Kipa Juma
Kaseja aliwapanga mabeki wake upande wa kulia kwake na mpira ulitua
kule, lakini akasahau upande wa kushoto ambao angekaa yeye, angalia
Kavumbagu alivyopiga kichwa chepesi na kuingia katika kona ya goli
ambapo hakukuwa na mlinzi yeyote, lile ni kosa kubwa”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi
aliyesisitiza kuwa jana alilazimika kufika uwanjani ili kujifunza zaidi
kuliko kutazama mpira kama shabiki wa kawaida aliongeza kuwa hata bao la
pili la Hamis Kiiza lilitiwa kambani kufuatia uzembe wa mabeki wa Simba
kushindwa kuosha mpira wa kona langoni kwao.
“Sisi
walimu huwa tunawafundisha wachezaji kuwa lazima beki aangalie mpira
utatua wapi na jinsi wachezaji wa timu pinzani alivyokaa (watch the
ball, watch the opponent players movement) , wakati kona inapigwa mabeki
wa Simba hawakuangalia wachezaji wa Yanga wamekaa vipi na hatari iko
wapi, mpira ulimkuta sehemu nzuri Kiiza na kufunga bao rahisi”. Alisema
kitaalamu Mwambusi.
Kocha huyo aliendelea kueleza kuwa walinzi wa Simba wanaocheza nafasi hiyo kiukweli asili yao siyo mabeki.
“Muangalie
Kapombe ambaye ni kiraka, anachezeshwa sehemu ya beki wa kati wakati
yeye anafanya vizuri zaidi pembeni, hata Musa Mude ni kiungo, lakini
mwalimu kalazimika kumchezesha nafasi ya ulinzi, ukiwaangalia mara
nyingi wanakosa mawasiliano mazuri na ndio maana jana wamepoteana sana”.
Alisema Mwambusi.
Akizungumzia
kikosi cha Simba, Mwambusi alisema watu wengi waliibeza klabu hiyo,
lakini yeye ameona kuwa Simba ina wachezaji bomba ambao kama watatunzwa
msimu ujao wa ligi watakuwa na timu bora zaidi.
“Wachezaji
vijana wamefanya kazi nzuri sana na wanaonekana kuwa makini na kutulia
sana, wakiendelea kuwa pamoja na kucheza kwa muda mrefu, Simba itakuwa
tishio”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi
alisema Simba kwa sasa bado ina matatizo na haijatengamaa ukilingaisha
na msimu uliopita, na hii inatokana na kushindwa kupata wachezaji
mbadala wa baadhi ya nyota wake waliotimka.
“Pengo la
Yondan bado lipo, Emmanuel Okwi, ma Marehemu Patrick Mafisango, hakika
kukosekana kwa wachezaji hawa imekuwa tatizo kubwa kwa Simba, nadhani
timu ipo wakati wa mpito na itawahitaji kutulia na kutengeneza kikosi
chake”.
Pia
alisema mechi ya jana imempa nafasi ya kujua falsafa za Soka la Simba na
Yanga hata kama wanaweza kubabili, hivyo inampa changamoto ya nini cha
kufanya akiwa na kikosi chake cha Mbeya City msimu ujao.
0 comments:
Post a Comment