Beki
wa Yanga anayevalia jezi nambari tatu, Stephano Mwasyika (kushoto)
akimiliki gozi la ng`ombe katika moja ya mechi alizoichezea Yanga
Stephano
Mwasyika (kushoto), Hamis Kiiza Diego (katikati) na Said Bahanuz
(kulia) wakishangilia moja la bao ambalo Yanga ilifunga mechi za Nyuma
Na Baraka Mpenja
Baada ya msimu wa ligi kuu kumalizika
mei 18, habari ya mjini kwa sasa ni vuguvugu la usajili, timu zimeanza
kutunishiana misuli. Jana Yanga wameanza kwa kumsajili Mrisho Ngassa.
Mtandao huu unaendelea kufanya jitihada
za kuwatafuta wachezaji mbalimbali ili kuzungumza nao juu ya maisha yao ya
baadaye na hali ya ligi ilivyokuwa.
Tumeanza na wachezaji wa Yanga ambao
wametwaa ubingwa, tuliongea na Frank Domayo, Nadir Haroub “Canavaro” na leo hii
tumekutana na beki wa kushoto wa Yanga, Stephano Mwasyika. Fuatilia mahojiano
na nyota huyo aliyekaa benchi kwa muda mrefu msimu huu;
MATUKIO DUNIANI: Stephano Mwasyika habari yako?
MWASYIKA: Safi! Habari ya kazi ndugu yangu?
MATUKIO DUNIANI: Salama
MWASYIKA: Nambie kaka?
MATUKIO DUNIANI: Hongera kwa kumaliza msimu wa ligi kuu soka Tanzania bara salama
salimini!
MWASYIKA: Asante sana, tunamshukuru Mungu
MATUKIO DUNIANI: Ubingwa wa mwaka huu ni wa pili kwako ukiwa na Yanga, unajisikiaje kwa
mafanikio hayo?
MWASYIKA: Daah! Nimefurahi sana kaka! Unajua mimi kama mchezaji siku zote naota
mafanikio, na baada ya kutwaa ubingwa mwaka huu huku tukiwafunga Simba mabao
2-0, ni faraja kwangu na famila yangu pia.
MATUKIO DUNIANI: Vipi mbona umesugua benchi sana msimu, uwezo wako umeshuka?
MWASYIKA: Hapana! Bado mimi nina uwezo mkubwa sana, nafanya mazoezi na timu, kila kitu kipo sawa. Kwanini sipangwi hiyo ni
ishu nyingine, kuna sababu binafsi ambazo siwezi kusema kwa sasa, lakini kuna
mipango nafanya, nikiweka sawa
nitakutaarifu tupige stori vizuri, kwasasa liache kaka!.
MATUKIO DUNIANI: Kwanini huwezi kusema?
MWASYIKA: Usiwe na shaka, nitakuambia tu, lakini kwa sasa liache kwanza, nikiweka
mambo sawa nitakuita nikupe mpango.
MATUKIO DUNIANI: Licha ya kutokucheza msimu huu, unakionaje kikosi cha Yanga?
MWASYIKA: Nafikiri kikosi ni kizuri, wachezaji wana uwezo mkubwa sana, kila mmoja
anajitahidi kutafuta nafasi ya kucheza. Ushindani ni mkubwa sana, nafikiri timu
itafanya vizuri sana michuano ya kimataifa.
MATUKIO DUNIANI: Yanga jana imemnasa Ngassa, unaonaje urejeo wa nyota huyo?
MWASYIKA: “That is good” ni bonge la mchezaji, namkubali sana. Ujio wake ni sahihi
na amerudi timu yake sahihi. Karibu sana Ngassa.
MATUKIO DUNIANI: Vipi kuhusu wewe, utasaini Yanga?
MWASYIKA: Ni mapema sana, nafikiri kuna mambo nayafanya kama nilivyokuambia awali,
ikifika muda wake nitakuambia wala usijali.
MATUKIO DUNIANI: Kwanini unaweka siri, kwani ni dhambi?
MWASYIKA: Nitakuambia bwana, subiri nijiweke sawa.
MATUKIO DUNIANI: Vipi ushindani wa ligi kuu msimu huu?
MWASYIKA: Ushindani ulikuwa mkubwa sana na kuna timu ambazo zimecheza vizuri
sana. Mimi nimeshuhudia timu zote, lakini timu ya Boniface Mkwasa, Ruvu
Shooting nafikiri imecheza kitimu zaidi na inajua kucheza, sema tatizo ni
kukosa kujiamini katika michezo yake. Pia Simba, Azam fc, Kagera, Coastal Union
zimecheza soka zuri sana na zinastahili sana kuwepo ligi kuu Tanzania bara.
MATUKIO DUNIANI: Siku zijazo timu hizi zinaweza kuondoa ufalme wa Simba na Yanga?
MATUKIO DUNIANI: Daaah! Siwezi kulisemea hilo, soka ni mipango, kama watawekeza vizuri
wanaweza kufanya vizuri na kuleta changamoto kwa timu za simba na Yanga.
Angalia Azam wanavyojitahidi sasa.
MATUKIO DUNIANI: Ligi umemalizika, unapumzika wapi safari hii?
MWASYIKA: Baada ya siku nne zijazo nataka kwenda nyumbani mkoani Mbeya kuwasalimia
wazazi. Kwa sasa nipo zangu geto maeneo ya Ilala. Karibu sana.
MATUKIO DUNIANI: Asante Mwasyika, nitafika huko tupige stori, kumbuka umesema kuna mambo
unayafuatilia halafu utatuambia!.
MWASYIKA: Tuko pamoja wala usijali, nitakuambia.
Mpenzi msomaji wa mtandao huu, haya ni
mazungumzo na beki wa kushoto wa klabu ya Yanga, Stephano Mwasyika.
Alisema kuna mambo anayafanya juu ya
mkataba, muda si mrefu atatujuza wapi anaelekea, je, Atabaki Yanga au anaihama
klabu hiyo?. Tusubiri.
Endelea kufuatilia habari hii hapa
hapa MATUKIO DUNIANI.
0 comments:
Post a Comment