Mwenyekiti
wa Kamati ya kuchunguza hesabu za Serikali (P.A.C) Omar Ali Shehe
akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wandishi wa habari kwa lengo la
kupata ushirikino na ufanisi katika utendaji wa kazi zao. Kikao hicho
kilifanyika Baraza la Wawakilishi Mbweni. Mkurugenzi
wa Mashtaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim akichangia katika kikao cha
Wadau mbalimbali wakiwemo wandishi wa habari wa vyombo tofauti kwa lengo
la kupata mashirikino na ufanisi katika utendaji wa kazi zao, (kulia)
Mhasibu Mkuu wa Serekali Omar Hassan, huko Baraza la Wawakilishi Mbweni.
Mwandishi
Salum Vuai, akitoa mchango wake kuhusu majukumu ya kamati ya kuchunguza
hesabu za Serekali. Kikao hicho kilifanyika Baraza la Wawakilishi
Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Ramadhani Ali-Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi
wa Mashtaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim amesema Serikali inawajibu
wa kuyafanyia uchunguzi wa kina mapendekezo ya Kamati za Baraza la
Wawakilishi na haipaswi kuwachukulia hatua moja kwa moja watu waliotajwa
ndani ya taarifa kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma.
Mkurugenzi
huyo ameeleza hayo leo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa pamoja
kati ya Kamati ya Uchunguzi wa Mahesabu ya Serikali na Mashirika (PAC)
na wadau wa Kamati hiyo kwenye Ofisi za Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Amesema
katika kuyapitia na kuyafanyia uchunguzi mapendekezo ya kamati,
wahusika wanaotajwa hupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuyatolea uamuzi
na kazi hiyo huchukua muda kukamilika.
“Serikali
haiwezi kuyachukulia hatua mapendekezo yote yanayotolewa na Kamati ya
Baraza bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea watuhumiwa na kubaini
wanaostahiki ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na wengine kupelekwa
mahakamani kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma”, alieleza Ibrahim
Mzee.
Ameitaka
Kamati ya PAC kuelewa kwamba kuna mchakato mkubwa unaotekelezwa na
Serikali kabla ya kuchukua hatua zinazostahiki kwa wahusika na haipaswi
kupewa shinikizo na chombo chochote.
Amesema
kazi ya Kamati ya PAC ni kuchunguza na kuishauri Serikali bila ya
kutumia vitisho wala kutoa hukumu na kuipa muda Serikali kufanya wajibu
unaostahiki ikiwa ni pamoja na kuwachukuliwa hatua waliobanika na
makosa.
Mkurugenzi
wa Mashtka alieleza kwamba kumekuwa na muingiliano wa kazi kati ya
kamati moja ya Baraza la Wawakilishi na Kamati nyengine na hivyo
kupelekea kamati mbili kuhoji jambo moja.
“Kamati
mbili ama zaidi kuhoji kitu kimoja ni kasoro kubwa hivyo inafaa
mujipange vizuri ili kila kamati ijuwe wajibu wake”, alisisitiza
Mkurugenzi wa Mashtaka.
Katibu
Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo
Khamis Mussa Omar ameitaka kamati ya PAC wanapowasilisha taarifa katika
Baraza kupunguza hamasa kwani mara nyingi hujenga picha kwa jamii kuwa
wahusika ni wizi na mafisadi.
Akiwashukuru
wadau wa PAC Mwenyekiti wa Kamati hiyo Omar Ali Shehe ameomba kujenga
mashirikiano ya karibu kati yao na wadau wengine ili kufanikisha
majukumu yao yao ya kazi.
Amewahakikisha
wadau hao kwamba Kamati ya PAC haina nia ya kumuonea Mtendaji yeyote
wa Serikali lakini kubwa wanalofanya ni kuhakikisha rasilimali chache
zilizopo Nchini zinawanufaisha Wananchi wote kwa mujibu wa nafasi zao.
Wadau
walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa mahesabu ya Serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Muhasibu Mkuu wa
Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka na Vyombo vya Habari.
0 comments:
Post a Comment