Na Baraka Mpenja
Baada ya
kukata tiketi ya kucheza michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu
wa 2013/2014, klabu ya Mbeya City chini ya kocha mwenye historia kubwa
ya kufundisha klabu ya Tanzania Prisons na timu ya mkoa wa Mbeya
“Mapinduzi Stars” kwa mafanikio makubwa Juma Mwambusi akisaidiwa na
kocha msaidizi Maka Mwalwisi imeanza mpango maalumu wa kusaka wachezaji
wapya kwa ajili ya mitanange ya ligi kuu msimu ujao.
Kocha
msaidizi wa klabu hiyo ambaye pia ni mkurugenzi wa kituo cha kuibua,
kulea na kukuza vipaji cha “Forest Youth Soccer Academy” (FOYSA) cha
jijini Mbeya, Maka Mwalwisi “Mnyambala wa kweli” ameimbia MATUKIO DUNIANI kuwa kuna wachezaji waliochaguliwa katika zoezi hilo la kutafuta wachezaji wa kujiunga na Mbeya City msimu ujao wa ligi kuu.
Mwalwisi
alisema wachezaji hao wanatarajia kucheza na timu ya ligi
kuu,”Wanankulukumbi” Kagera Sugar siku ya jumapili (mei 19) wilayani
Kyela.
“Baada ya
Kagera Sugar kucheza na Prisons mei 18 mwaka huu uwanja wa Sokoine,
tumewaomba kucheza dhidi ya kikosi chetu ambacho tumekiandaa ili
kutafuta wachezaji wapya, mechi hiyo itatusaidia kujua wachezaji gani
wanatufaa ili tuwasajili”. Alisema Mwalwisi.
Mdau huyo
mkubwa wa soka la vijana aliongeza kuwa katika kikosi hicho wachezaji
wengi ni vijana na wapo katika umri sahihi wa kucheza mpira ikizingatiwa
kuwa soka la kisasa linahitaji makinda wengi zaidi kuliko wakongwe
“Mafaza”.
“Kagera
sugar ni timu nzuri na ina mwalimu mzuri, vijana wetu watapata funzo
kubwa kutoka kwao, sisi benchi la ufundi la Mbeya City tunaamini kuwa
itakuwa nafasi barabara kwetu kuwatazama vijana wetu”. Alisema Mwalwisi.
Mbeya City
imekata tiketi ya kucheza ligi kuu msimu ujao baada ya kufanya vizuri
zaidi katika michuano ya ligi daraja la kwanza msimu wa mwaka huu.
Mbali na
kukata tiketi mwaka huu, msimu uliopita pia walibakia kidogo kufuzu
lakini bahati ikaangukia kwa upande wa mahasimu wao wajela jela Tanzania
Prisons.
Sasa
kutakuwepo na “Mbeya Derby” baada ya Prisons kubakia ligi kuu, huku
Mbeya City nao wakiwa tayari wameshatinga michuano hiyo.
Kagera
Sugar wanatarajiwa kuwasili kesho jijini Mbeya kujindaa na mchezo wa
jumapili dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons mei 18 mwaka huu katika
uwanja wa Sokoine.
0 comments:
Post a Comment