Mhe. Dkt.
Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi; Mhe Abbasi Kandoro,
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya;
Ndugu M.A.K Mringo,
Mwenyekiti wa TAMONGSCO;
Bw. Joseph Patel, Rais wa
Shirikisho la Shule Zisizo za Serikali za Malawi (ISAMA);
Mwakilishi wa Benki ya Afrika;
Viongozi na Watendaji waiki
na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Shukrani
Nakushukuru sana
ndugu Mringo, Mwenyekiti wa TAMONGSCO na viongozi wenzako kwa kunialika na kunishirikisha
kwenye mkutano huu muhimu wa taasisi yenu. Nimefurahishwa na kauli mbiu yenu inayosema “Changamoto na fursa zilizopo katika
ushirikiano baina ya sekta ya umma na isiyo ya umma katika utoaji wa elimu
bora”. Ni kauli mbiu muafaka kabisa
kwani ili elimu nchini iweze kuwa bora hatuna budi kuzitambua changamoto
zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.
Maendeleo maana yake ni kuzitafutia ufumbuzi changamoto au mambo
yanayokuwa vikwazo vya maendeleo. Mimi
na wenzangu tunasubiri kwa hamu mapendekezo ya kuondoa changamoto hizo
mtakayoyatoa mwishoni mwa mkutano wenu.
Pamoja na hayo napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tunatambua
na kuthamini sana ushirikiano uliopo baina yake na ninyi wamiliki na
waendeshaji wa shule binafsi nchini. Kwa namna ya pekee nawapongeza sana kwa namna
ambayo mnashirikiana na Serikali kuendeleza elimu nchini. Tutafanya kila tuwezalo kuudumisha na
kuuboresha ushirikiano wetu huu.
Umuhimu wa Elimu
Ndugu Mwenyekiti;
Tangu uhuru wa nchi yetu, maendeleo ya
elimu imekuwa suala kubwa na la kipaumbele cha juu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitaja
maadui watatu wa maendeleo ya taifa letu kuwa ni ujinga, umaskini na
maradhi. Bado hao wameendelea kuwa
maadui wa maendeleo yetu mpaka sasa. Sera, mipango na mikakati mbalimbali
inayobuniwa na kutekelezwa nchini tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza mpaka hii
ya Awamu ya Nne ina shabaha ya kuwashinda maadui hao.
Ninyi na mimi ni mashahidi kuhusu mafanikio tuliyoyapata na tunayoendelea
kupata katika vita hivi. Hata hivyo,
bado tunayo safari ndefu mbele yetu.
Tena safari hiyo ina milima mirefu ya kupanda na miteremko mikali. Kukabiliana na changamoto hizo ni jukumu la
Serikali, wananchi na wadau mbalimbali
wa hapa nchini na hata nje ya nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan TAMONGSCO imeongeza sana uwekezaji
katika maendeleo ya elimu nchini.
Matokeo yake ni kuwa tumepanua sana fursa za elimu ya awali, msingi,
sekondari, ufundi na elimu juu. Hivi
sasa tunao watoto 1,034,729 katika madarasa
ya awali jambo ambalo halikuwepo wakati wa ukoloni. Ni Sera ya Serikali kwamba kila shule ya msingi iwe na madarasa
ya awali sera ambayo imekuwa inatekelezwa vizuri.
Kwa upande wa elimu ya msingi idadi
ya wanafunzi imeongezeka kutoka 486,470
mwaka 1961 hadi 8,247,172 mwaka 2012. Hivyo hivyo, kwa upande wa elimu ya sekondari
ambapo idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 1,884,272
mwaka 2012. Kwa upande wa elimu ya juu
tumetoka kuwa nchi isiyokuwa na chuo kikuu hata kimoja na wahitimu wasiozidi 10 hadi kuwa na vyuo vikuu 48 vyenye wanafunzi 166,484 mwaka 2012.
Ndugu Mwenyekiti;
Haya ni mafanikio makubwa sana na ya kujivunia. Maendeleo ya elimu tangu uhuru mpaka sasa
yalipitia hatua mbalimbali. Tulirithi
kutoka ukoloni mfumo wa elimu ambao Serikali Kuu haikuwa imejihusisha vya
kutosha na ujenzi wa shule na kuwapatia wananchi elimu. Hilo liliachiwa Serikali za Mitaa (Native
Authority), Wamisionari na wananchi wenyewe pale ambapo walikuwa na mwamko wa
elimu. Baada ya uhuru, Serikali Kuu
ikaanza kujihusisha kwa ukamilifu katika ujenzi na uendeshaji wa shule. Ilitaifisha shule za mashirika ya dini na
kujenga nyingine. Mwaka 1974,
ukaanzishwa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE) uliowezesha upanuzi mkubwa
wa elimu ya msingi kwa kila kijiji kuwa na shule yake. Mwaka 2005, Serikali iliamua kuanza upanuzi
mkubwa wa elimu ya sekondari kwa ujenzi wa shule za sekondari kwa kila Kata. Tulilazimika kufanya hivyo kwa sababu fursa
za vijana wanaomaliza elimu ya msingi kuendelea na elimu ya sekondari zilikuwa
finyu mno.
Mwaka 1998, Serikali ilifanya uamuzi wa msingi wa kutoa fursa kwa sekta
binafsi kuwekeza katika maendeleo ya elimu nchini. Uamuzi huo ulitokana na kutambua ukweli kuwa
Serikali ikishirikisha na kushirikiana na sekta binafsi itasaidia sana kupanua
fursa za elimu nchini. Napenda kutumia
nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa sekta binafsi kwa kuupokea vizuri uamuzi
huo na kuchukua hatua thabiti na kuwekeza katika ujenzi wa shule za awali,
msingi na sekondari pamoja na vyuo vya ufundi, ualimu na elimu ya juu. Ni ukweli ulio wazi kuwa mchango wa sekta
binafsi umeliwezesha taifa kupata
mafanikio tunayojivunia leo.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa kazi nzuri
iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na sekta binafsi katika maendeleo ya elimu
nchini. Mmekuwa mnatoa mchango mkubwa na
wenye manufaa makubwa kwa taifa.
Nawashukuru kwa kupanua fursa za elimu kwa Watanzania na hasa kwa ubora
wa elimu inayotolewa. Nawaomba muendelee
na moyo huo. Nawahakikshia ushirikiano
wangu na ule wa Serikali ili kuwawezesha mtekeleze malengo yenu.
Majibu ya Risala
Ndugu Mwenyekiti;
Mchakato wa kutunga Sera Mpya ya Elimu
baada ya ile ya mwaka 1995, umefikia katika hatua za mwisho. Kinachosubiriwa sasa ni maoni ya Wabunge ili
Sera ikamilishwe. Naamini kabla ya
mwisho wa mwaka huu Sera itakuwa tayari kutumika. Tunaamini kuwa Sera hiyo mpya italeta
mabadiliko katika uendeshaji wa mifumo yetu ya elimu hapa nchini. Itatoa majibu kwa maswali mengi
mliyoyauliza. Aidha, nafasi ya sekta
binafsi katika kuchangia maendeleo ya elimu nchini itafafanuliwa kwa upana na
kina zaidi.
Wakati huo huo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya
Elimu Tanzania itaanza maandalizi ya kupitia upya mitaala ya elimu nchini ili
nayo ilingane na malengo ya Sera Mpya ya Elimu.
Mitaala itakayoenda sambamba na hali ya sasa na mahitaji ya maendeleo
nchini na duniani. Napenda
kuwahakikishia kuwa kutakuwepo na ushirikishaji wa wadau mbalimbali, wakiwemo
wa sekta binafsi katika zoezi hilo.
Ndugu Mwenyekiti;
Uimarishaji wa Idara ya Ukaguzi wa
Elimu nchini utapewa kipaumbele cha juu.
Tunatambua kuwa hali ilivyo sasa hairidhishi hata kidogo na kwamba zipo
changamoto nyingi ambazo lazima zipatiwe ufumbuzi. Serikali imeanza na inaendelea kuchukua hatua
thabiti za kuimarisha ukaguzi wa shule na vyuo hapa nchini. Miongoni mwa mambo yanayofikiriwa kufanywa ni
kuibadili Idara ya Ukaguzi kuwa taasisi inayojitegemea na kuiwezesha kwa rasilimali
watu, vitendea kazi na fedha. Naamini tutaimarisha
utendaji wa kazi ya ukaguzi na matokeo yake yataonekana kwa muda mfupi.
Pamoja na juhudi hizo, napenda kuwakumbusha kuwa Mkaguzi wa kwanza wa shule
ni Mkuu wa Shule. Yeye ndiye mwenye
jukumu la kuhakikisha shule anayoiongoza inafuata miongozo iliyopo na inakidhi
viwango vya ubora vilivyowekwa. Naomba
jukumu hili mlitekeleze ipasavyo.
Wamiliki ndiyo wakaguzi wakuu wa kwanza.
Ndugu Mwenyekiti;
Mabibi na Mabwana;
Nimesikia kilio chenu kuhusu
utekelezaji wa sheria za kodi na gharama za kibali cha mgeni kufanya kazi
nchini. Kuhusu kodi, tutaangalia namna
ya kupunguza urasimu katika utoaji wa misamaha ya kodi iliyoruhusiwa kisheria. Tutazielekeza mamlaka zinazohusika yaani
Hazina na TRA kuweka mfumo mzuri katika kutekeleza wajibu wake. Ninawaomba na nyie mhakikishe kuwa taarifa
zinazotakiwa zinatolewa kwa usahihi.
Wakati mwingine usumbufu mnaoupata unatokana na hoja ya TRA kujiridhisha
kabla ya kutoa misamaha. Bila hivyo,
taasisi zisizostahili zitajipenyeza kwa nia ya kujinufaisha kinyume cha sheria. Nakubaliana nanyi kuwa ipo haja ya kupitia
upya tozo ya vibali vya kufanya kazi kwa waalimu kutoka nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, hususan wa fani ambazo tunao upungufu mkubwa.
Ndugu Mwenyekiti;
Nimesikiliza kwa makini sana hoja yenu
ya kutaka kushirikiana na Serikali kuondokana na msongamano wa wanafunzi katika
baadhi ya shule zake. Natambua kwamba
wakati Serikali inahangaika kupunguza msongamano katika shule zake, baadhi ya
shule zenu zina madarasa yaliyo wazi na zingependa kuletewa wanafunzi na
Serikali. Pamoja na uzuri wake, suala
hili lina changamoto zake kutokana na ukweli kwamba gharama katika shule zenu
ni kubwa hivyo wazazi au Serikali
hatutaweza kumudu.
Ndugu Mwenyekiti;
Ninalo ombi moja kwenu ambalo napenda
mlijadili kwenye mkutano wenu. Ombi
lenyewe sio geni, linahusu ada kubwa zinazotozwa na shule au vyuo vyenu. Wapo wananchi wengi ambao wangependa sana
kunufaika na elimu nzuri mnayoitoa lakini wanashindwa kutokana na ada inayotozwa
kuwa kubwa. Sisemi ada zenu zifanane na
za shule za Serikali, lakini baadhi ya shule na vyuo vyenu vinalalamikiwa na
wananchi kwa kutoza ada kubwa na kwamba hazitabiriki kwani hupandishwa wakati
wowote.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi imeliona hilo, na imeamua kulifanyia kazi . Tathmini ya gharama halisi za uendeshaji kwa
mwanafunzi (student unit cost) itafanywa ili kutoa ushauri stahiki kwa wamiliki
wote wa shule au vyuo kuhusu kiwango. Elimu
ni huduma muhimu na haki kwa mtoto. Si
vyema kugeuzwa kuwa ni biashara ya kuleta faida kubwa. Hadi sasa uthamini kwa
vyuo vya elimu ya juu imeshafanyika na mapendekezo ya gharama halisi
yameandaliwa. Aidha, hatua za kumpata
mtaalamu elekezi zimefanyika kwa ajili ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa shule a sekondari.
Ahadi ya Serikali
Ndugu Mwenyekiti;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali
itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana wengi
zaidi wa Kitanzania kupata elimu.
Tutaendelea kupokea na kufanyia kazi ushauri wenu ili kuboresha zaidi
mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu.
Mambo mliyoyaeleza katika risala yenu nimeyasikia. Na tutayafanyia kazi. Mengine tulishayazungumza na viongozi wenu
kabla ya kuja hapa. Watawaeleza kwa
kirefu. Naomba mfanye jitihada zaidi
kujenga shule za mafunzo ya ufundi na stadi za kazi. Wahitimu wa shule hizi wanapata kazi kirahisi
katika soko la ajira na wanaweza kujiajiri wenyewe kwa urahisi.
Pongezi Kwa Wizara na Wamiliki wa Shule na Vyuo
Kabla ya kumaliza napenda kutambua na
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Naibu wake, Katibu Mkuu na
wafanyakazi wote wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa juhudi zao za
kusimamia sekta ya elimu nchini. Ni kazi
ngumu, yenye changamoto zake nyingi, hususan katika kipindi hiki ambacho
mahitaji ya elimu ni makubwa sana.
Lakini wenzetu hawa wanatekeleza majukumu yao kwa bidii na maarifa. Asanteni sana.
Nawashukuru pia wamiliki wa shule na
vyuo kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha Watanzania. Naomba muendelee kuwa mstari wa mbele
kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu, miongozo mbalimbali iliyotolewa pamoja
na sheria zinazosimamia utoaji na uendeshaji wa elimu nchini. Kazi ya kutoa elimu kwa Watanzania ni yetu
sote. Tuifanye kwa umakini na weledi wa
hali ya juu.
Mwisho
Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.
Asanteni kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment