Na Baraka Mpenja
Kuwepo
kwa mfumo dume, kukosa nia ya uthubutu, mazingira ya rushwa na kutojali
soka la wanawake imeelezwa kuwa ndio sababu kubwa ya wanawake wengi
nchini Tanzania kutoshirikia katika michezo kwa maana ya kucheza na
kuongoza taasisi za michezo mfano TFF.
Hayo
yameelezwa na aliyewahi kuwa makamu wa mwenyekiti wa chama cha riadha
Tanzania (RT) miaka ya 1976, mjumbe wa kamati ya wanawake na Uchaguzi ya
TFF, na sasa mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu yaYanga ya Dar es
salaam, Bi. Sara Ramadhan katika mahojiano maalumu na mtandao wa MATUKIO DUNIANI.
Bi.
Sara amesema wanawake wanapolundikiwa majukumu ya nyumbani kama kufua,
kupika, kulea watoto n.k Kumesababisha wengi kutoshiriki katika michezo
kwa maana ya kucheza na kujihusisha na mambo ya kuongoza michezo.
Mdau
huyo wa soka aliongeza kuwa mbali na mfumo wa kumtumikisha mwanamke
katika majukumu mengi ya kifamilia, pia mazingira ya rushwa katika
chaguzi mbalimbali imekuwa tatizo kubwa kwa wanawake kupata nafasi za
uongozi katika taasisi za soka nchini.
“Unajua
katika chaguzi nyingi kuna matumizi ya pesa nyingi ambazo ni rushwa kwa
namna moja ama nyingine, kiukweli ni ngumu sana kwa mwanamke kumwaga
pesa ili achaguliwe, mara zote anawaza kuwalea watoto wake, mume wake na
ndugu zake wa nyumbani, na ndio maana kupata nafasi za juu imekuwa
ngumu sana”. Alisema Bi Sara.
Sara
alisisitiza kuwa imekuwa ngumu sana kwa wanawake kuaminiwa na kupewa
nafasi za juu katika taasisi za soka na hivyo kushindwa kuwahamasisha
wanawake wengine kuingia katika mipango ya kuendeleza soka la Tanzania.
Mbali
na tatizo hilo, Sara aliendelea kueleza kuwa wanawake wamejiweka mbali
sana na masuala ya michezo kutokana na kukosa nia ya uthubutu.
“Wanawake
wengi hawaamini kama wanaweza, na ndio maana katika chaguzi nyingi
hawajitokeza, lakini kwangu mimi hata TFF fomu za kuomba nafasi nitajaza
kwasababu najiamini sana”. Alisema Bi Sara.
Akizungumzia
suala la soka la wanawake, Bi Sara alisema TFF imeshindwa kuwekeza
katika soka hilo na ndio maana hakuna ligi za soka kwa wanawake katika
mikoa ukiachana na Dar es salaam.
“Leo
hii unaibuka na kusema unataka kuendeleza soka la wanawake, jamani
unaanzia wapi?, hakuna ligi wala nini, hakika ni ngumu sana kufikia
malengo yetu”. Alisema Bi Sara.
Bi
Sara alipoulizwa kama soka letu linaendelea tofauti na miaka ya nyuma,
alisema yeye anaenda tofauti na watu wengi wanaodhani soka letu
linaendelea.
“Huwezi
kusema soka linakua kama huwekezi soka la vijana, nani anajua jinsi
timu ya taifa inavyochaguliwa?, kwanini Yanga, Simba na Azam?, hakuna
mchakato wa kuzunguka mikoani kutafuta vipaji vipya, kwa hali hii
tutabaki kujiona tunaendelea kumbe tuko palepale”. Alisema Bi Sara.
Aidha
Bi Sara alishauri kuwa ni lazima kila mkoa uwe na vituo vya soka la
vijana kuanzia saba au nane ambavyo vinasaidiwa na TFF kupata vifaa vya
michezo na kutumika kama vitalu vya kupata timu za vijana za taifa na
timu ya wakubwa kama ilivyo kwa nchi za wenzetu.
0 comments:
Post a Comment