Na Boniface Wambura
KLABU ya Barrack Young Controllers II ya Liberia imewasili nchini leo asubuhi na kufikia katika hoteli ya Sapphire Court, kariakoo, Dar es Salaam tayari kwa mechi ya marudiano ya Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Azam itakayochezwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Young Controllers imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 3.35 asubuhi ikitokea Nairobi, Kenya ilipounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.
Imetua na msafara wa watu 37 wakiwemo wachezaji 21, ukiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo, Robert Alvin Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.
Wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy, Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.
Benchi la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu, Robert Lartey akisaidiwa na Samuel Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel Massaquoi.
Timu hiyo inatarajia kundoka kurejea Monrovia, Aprili 8 mwaka huu kupitia Nairobi, Kenya saa 11.10 alfajiri kwa ndege.
Azam ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza mjini Monrovia wiki mbili zilizopita na sasa inahitaji hata sare katika mchezo wa Jumamosi ili kusonga mbele.
Hoteli ua Sapphire imejizolea umaarufu mkubwa kwa sasa nchini kwa timu mbalimbali kufikia hapo zinapokuja kwenye mechi mbalimbali.
Hoteli hiyo imepitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwamba ipo katika viwango vya bora vya kukidhi mahitaji ya timu zinapokuja nchini.
0 comments:
Post a Comment