TIMU ya Azam FC, inatarajia kuingia kambini keshokutwa kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), dhidi ya Barrack YC ya Liberia, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Jumamosi.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa ugenini, Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Azam FC, imefuzu hatua hiyo baada ya kuiondosha Al Nasri Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Msaidizi wa Azam FC, Jemedari Saidi, alisema hiyo ni mechi muhimu kwao katika kuhakikisha wanasafisha njia ya kuelekea ubingwa wa kombe hilo na kuweka historia hapa nchini.
“Timu itaanza mazoezi rasmi kesho, lakini kambini ni Jumatano ambapo kikosi kitaongezewa nguvu na Brian Umony ambaye alipumzishwa katika mechi ya jana (juzi) ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting,” alisema Jemedari.
Katika hatua nyingine, kiungo mkabaji wa timu hiyo, Abdulhalim Humud, ametua salama nchini Afrika Kusini alikokwenda kufanya majaribio katika klabu ya Jomo iliyoko Ligi Daraja la Kwanza na tangu juzi ameanza majaribio hayo.
Jemedari alisema kwa mujibu wa mmiliki wa timu hiyo, ameshangazwa na Humud kukosa namba katika timu ya Azam, kwa jinsi alivyomuona anacheza tangu afike katika timu yake.
Alisema kutokana na sifa zilizotolewa na mmiliki huyo, ana uhakika Humud huenda akasajiliwa na timu hiyo ambayo inapigania kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
BARRACK YC |
0 comments:
Post a Comment