
![]() |
TANZANIA PRISONS |
Na Baraka Mpenja
Maafande wa jeshi la magereza, Tanzania Prisons “wajelajela” wapo kambini kujiandaa na mchezo
wa mei mosi dhidi ya wanapiga kwata wenzao wa JKT Ruvu wanaohaha kutafuta njia
ya kubakia ligi kuu msimu huu. Mtanange huo utapigwa uwanja wa Chamazi Mbande nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam majira ya saa 10 kamili jioni.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Mbeya, katibu
mkuu wa klabu hiyo Sadick Jumbe alisema wao wanajifua vilivyo huku wakichagizwa na ushindi
wa mechi mbili mfulululizo katika dimba la nyumbani la kumbukumbu ya Hayati
Edward Moringe Sokoine jijini humo.
“Mwalimu Jumanne Chale anaendelea kunoa makali ya vijnana
wetu, tunajua wenzetu JKT Ruvu wapo katika hali mbaya na wana mechi ngumu kesho
dhidi ya Yanga, wiki ijayo wanacheza na Lyon na baada ya hapo watakutana na
sisi Chamazi, hakika wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kwani mechi zote ni ngumu
sana na sisi tuko barabara sana”. Alisema Sadick Jumbe.
Jumbe alisema kikosi kizima kipo sawa, vijana wana morali
kubwa kujiandaa na mchezo huo ambapo aprili 28 wataanza safari ya kuelekea Dar
es salaam tayari kwa matanange huo dhidi ya maafande wa Ruvu JKT ambao mpaka
sasa hawana kocha mkuu baada ya kocha wake Charles Kilinda kubwaga manyanga kuinoa
klabu hiyo.
“Nilisema toka awali kwamba mtu akifikisha pointi 26 angalau
anakuwa katika hali nzuri, sisi tuna uhakika wa kubakia ligi kuu msimu huu,
kila mechi kwetu muhimu sana na Ruvu JKT watambue kuwa wanakutana na wanaume
wenzao ambao wako kamili kila idara kusaka ushindi”. Alijigamba Jumbe.
Katibu huyo aliongeza kuwa kamati ya saidia Prisons ibaki
ligi kuu chini ya kamanda wa polisi mkoani humo, Diwani Athman Msuya
akishirikiana na viongozi wa serikali pamoja na wadau wa soka imeleta hamasa
kubwa na mshikamano katika kikosi chao kwani wachezaji wanajisikia furaha sana
kushangiliwa na umati mkubwa wa watu.
“Hakika sasa wana Mbeya wameamua kutusaidia kwa hali na mali
na ndio maana siku za karibuni timu imekuwa na ari kubwa katika mechi
zilizopita, moto huu tutauendeleza mwanzo mwisho ili kupata ushindi na kujiweka
nafasi nzuri zaidi”.
Katika mechi mbili zilizopita, Prisons iliwatungua bao 1-0 Mgambo
JKT na ikashusha kipigo cha mabo 2-0 kwa vijana wa Charles Boniface Mkwasa,
klabu ya Ruvu Shooting kutoka mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
Endapo Prisons itafanikiwa kubakia ligi kuu msimu huu, msimu
ujao wa ligi kuu Tanzania bara mkoa huo utakuwa na timu mbili zinazowakilisha
wapenda mchezo wa soka jijini humo, klabu hizo zitakuwa Mbeya City chini ya
kocha Juma Mwambusi na Prisons chini ya Jumane Chale.
0 comments:
Post a Comment